Date: 
12-02-2025
Reading: 
Luka 6:1-5

Hii ni Epifania 

Jumatano asubuhi tarehe 12.02.2025

Luka 6:1-5

1 Ikawa siku ya sabato moja alikuwa akipita katika mashamba, wanafunzi wake wakawa wakivunja masuke na kuyala, wakiyapukusa-pukusa mikononi mwao.

2 Basi baadhi ya Mafarisayo wakawaambia, Mbona mnafanya lisilo halali siku ya sabato?

3 Yesu akawajibu akawaambia, Hamkulisoma hata hilo alilolifanya Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wale aliokuwa nao?

4 Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaitwaa mikate ile ya Wonyesho, akaila akawapa na hao wenziwe, ambayo si halali kuila ila kwa makuhani peke yao.

5 Akawaambia, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.

Utukufu wa Mwana wa Mungu;

Ni siku ya Sabato, Yesu yuko na wanafunzi wake akiendelea na utume wake. Ilifika mahali akapita eneo la mashamba, wanafunzi wakaanza kuvunja masuke (sehemu ya nafaka inayotoa ua na mbegu) na kula. Mafarisayo kwa sababu ya kuishika torati waliona siyo sahihi, wakamwambia Yesu na wanafunzi wake kuwa jambo hili siyo sahihi

Yesu katika kuwajibu anawakumbusha juu ya Daudi aliyeumwa na njaa akatwaa mikate na kula, tena iliruhusiwa kwa makuhani tu! Yesu anarejea hapa;

1 Samweli 21:5-6

5 Naye Daudi akamjibu kuhani, akamwambia, Hakika tumejitenga na wanawake siku hizi tatu; napo nilipotoka, vyombo vya vijana hawa vilikuwa vitakatifu, ingawa ilikuwa safari ya sikuzote; basi leo je! Vyombo vyetu havitakuwa vitakatifu zaidi?
 
6 Ndipo kuhani akampa ile mikate mitakatifu; kwa maana hapakuwa na mikate ila ile ya Wonyesho, nayo imekwisha kuondolewa mbele za Bwana, ili itiwe mikate ya moto siku ile ilipoondolewa.

Mkazo wa Yesu ni kuwa yeye ndiye Bwana wa sabato. Kumbe Yesu Kristo ndiye Mwokozi wetu. Mwamini sasa uokolewe. Amina

Siku njema

Heri Buberwa