Date:
07-01-2025
Reading:
Isaya 60:1-3
Hii ni Epifania.
Jumanne asubuhi tarehe 07.01.2025
Isaya 60:1-3
[1]Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja,
Na utukufu wa BWANA umekuzukia.
[2]Maana, tazama, giza litaifunika dunia,
Na giza kuu litazifunika kabila za watu;
Bali BWANA atakuzukia wewe,
Na utukufu wake utaonekana juu yako.
[3]Na mataifa wataijilia nuru yako,
Na wafalme kuujia mwanga wa kuzuka kwako.
Yesu ni Nuru ya Ulimwengu
Leo asubuhi tunaendelea kukumbuka kung'aa kwa Yesu, kama tulivyosikia katika ibada ya jana.
Ukisoma Somo la leo asubuhi, kabla yake, yaani Isaya 59, ni mwendelezo wa utabiri wa kuzaliwa kwa Yesu. Yesu anatabiriwa kuja, kuondoa uovu na udhalimu.
Baadae, katika somo la asubuhi hii tunaona Isaya akiongelea "kusanyiko jipya la waliotawanyika". (angalia mstari wa 4) Isaya anamtabiri Yesu kama Nuru ya Ulimwengu, inayokuja kuuangazia Ulimwengu wote.
Katika Agano jipya, Nuru hii ni Yesu Kristo;
Luka 1:78-79
[78]Kwa njia ya rehema za Mungu wetu, Ambazo kwa hizo mwangaza utokao juu umetufikia, [79]Kuwaangaza wakaao katika giza na uvuli wa mauti, Na kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani.Hata Mtume Paulo anakiri hilo;
Waefeso 5:13-14
[13]Lakini yote yaliyokemewa hudhihirishwa na nuru maana kila kilichodhihirika ni nuru. [14]Hivyo husema, Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza.Giza linawakilisha dhambi, na Nuru inawakilisha Utakatifu. Sisi tulio wadhambi, tukimkaribisha Yesu tunaondokana na dhambi (Giza) na kuivaa Nuru ambayo ni utakatifu /wokovu. Tunaitwa kuwa watoto wa Mungu, tuipokee Nuru hii, iongoze maisha yetu. Utukufu wa Mungu utaonekana kwetu, tukimpokea Yesu, ambaye ni Nuru ituangazayo.
Uwe na siku njema
Heri Buberwa
Mlutheri