Date:
04-12-2024
Reading:
Mathayo 24:42-44
Hii ni Advent
Jumatano asubuhi tarehe 04.12.2024
Mathayo 24:42-44
[42]Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu.
[43]Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa.
[44]Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja.
Bwana analijia Kanisa lake;
Yesu anatukumbusha kukesha (42) maana hatujui siku atakayorudi. Kwa maana nyingine, anatukumbusha kuwa katika yote tufanyayo, tuchukue "tahadhari" kwa mambo ambayo yanaweza kutuzuia kuuona ufalme wake. Kuchukua tahadhari ni onyo linalotokea sana kwenye sura ya 24, na ni daraja linalounganisha mifano yote inayotuelekeza kuwa "makini", "kujiandaa" na kuchukua "tahadhari"
Kitenzi cha Kiyunani "gregoreo" hutafsiriwa "tahadhari" katika maandiko na kimetumika mara 22 katika Agano jipya la Kiyunani. Kitenzi hiki kinaleta wazo la "kuwa macho", "kuwa makini". Alitumia Yesu neno hili alipokuwa akiomba Gethsemane wanafunzi wake wakilala; Mt 26:38,40,41, Mk 14:34, 37,38. Katika somo la asubuhi ya leo, maudhui ya kuwa macho pia yanapatikana katika mstari wa 43 (kukesha). Maandiko yanaeleza kuwa wasioamini hawatakuwa na tahadhari, hivyo hawataujua ujio wa Yesu kwa mara ya pili (Soma 1Thes 5). Mtume Paulo anaonesha kuwa waliochukua tahadhari hawatashtuka, maana watakuwa wamejiandaa kwa ujio wake. Hata Yohana alifunuliwa;
Ufunuo wa Yohana 16:15
[15](Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.)Ufunuo huu unatuonesha kuwa ni muhimu kumngoja Bwana, kwa umakini mkubwa, kwa tahadhari.
Fundisho hili la Yesu leo asubuhi linatukumbusha kuwa waaminio watamuona Bwana akirudi, maana watakuwa wamejiandaa na kuchukua tahadhari. Ndiyo maana katika mstari wa 44 Yesu anatuita kujiweka tayari kumngojea. Israeli haikuwa imejiandaa wakati wa kuja kwa Yesu mara ya kwanza, lakini waliosalia lazima wawe tayari na wajiandae kumlaki Bwana. Binafsi naweza kusema Israeli walimpokea Yesu "kizembe", kitu ambacho Yesu hataki sisi tufanye.
Maudhui makuu katika somo la asubuhi ya leo, yaani kuwa tayari, ni kumpokea Yesu, na kuwa tayari kumlaki Bwana kama Mfalme, na siyo mwamuzi. Yesu alikuwa akiwaambia Israeli kujiandaa kumpokea kama Mfalme arudipo mara ya pili. Kujiandaa ni pale mtu ampokeapo Yesu kama Mesiya.
"...somo liko wazi. Mwenye nyumba akijua saa ya mwizi ajapo, hujiandaa kumkabili. Kwa maana hiyo, waaminio sharti wawe tayari. Ishara za siku hizo zitawaonesha kuwa kurudi kwake ni karibu..."(Stanley Toussaint)
Kwa nini tukeshe?
1.Ufalme wa Mungu ulikuwepo
Ufalme wa Mungu upo
Ufalme wa Mungu utakuwepo. Hivyo, kama Yesu alivyokuja, atarudi tena kulichukua Kanisa. Kwa ukweli huu ni lazima kila mmoja wetu ajiandae kumpokea. Ufalme wa Mungu ulikuwepo, upo na utakuwepo (realised eschatology)
2.Hatujui lini Yesu atarudi.
Yesu anatuita kuiweka mioyo yetu mbali na uharibifu wa aina yoyote katika imani. Maigizo ya maisha hayafai, bali maisha halisi ya kumwamini Yesu na kumfuata kwa utimilifu kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Msisitizo wa Yesu ni kukesha. Kukesha kwa leo tunakofundishwa siyo kulala macho wazi, bali kukaa katika imani pasipo kuyumba, siku zote bila kuchoka. Huu ndio mkesha halisi. Kukesha kwa leo siyo kulala macho wazi. Kulala macho wazi wakati mioyo siyo safi ni kupoteza muda. Ni vizuri kuutumia usiku kumtafuta Mungu (kukesha) lakini roho zetu zikiwa safi. Wewe unakesha?
3.Asiyekesha huibiwa.
Hapa tusimamie mstari wa 43.
Yesu alitumia mfano wa wenye nyumba ili kueleweka zaidi. Ni wazi kuwa alilenga sote kuelewa, maana unaweza kuwa humiliki nyumba, lakini unalala kwenye nyumba hapohapo ulipo. Ikitokea ukajua mwizi atakuja lazima utakuwa tayari kumkabili. Mwizi anaogopesha. Wengine wanaiba, wengine wanapiga na kuiba, wengine kuua kabisa! Kwa sababu ya maendeleo na Teknolojia, siku hizi mtu akipata taarifa kama hiyo, atalifaarifu jeshi la polisi kwa ajili ya msaada. Ni kwa sababu mtu huyo anajua hawezi kumfukuza mwizi bila msaada!
Nimesema mwizi huogopesha. Kwa maana hiyo, mambo yanayotukwamisha kuwa karibu na BWANA yanaogopesha, ni ya kuacha, tusiyape nafasi. Kama nilivyosema, huwezi kupambana na mwizi, siyo rahisi. Vivyo hivyo, huwezi kupambana na dhambi kwa nguvu zako, bali kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Alindaye mwizi hukesha, naam, tunahitaji kushinda dhambi wakati wote, maana BWANA analijia Kanisa lake.
Sasa basi;
Haitegemewi mkristo wa kweli kulazimishwa kumpenda na kumwamini Yesu. Ni wajibu wa mkristo kutambua upendo wa Yesu aliyekuja, aliyepo na atakayekuja, katika njia ya ufuasi. Tunapopendana sisi kwa sisi huwa tunajitahidi kuonyeshana kwa vitendo jinsi upendo wetu ulivyo miongoni mwetu. Kwa nini tusimwonyeshe Yesu kumpenda? Kumwonyesha Yesu kuwa tunampenda ni kumwamini, kumpokea na kumfuata kwa mioyo yetu yote, kuelekea uzima wa milele. Tukimpenda tunafanya yaliyo ya kweli, yaani tunatenda mema kwa utukufu wa jina lake. Nini tunafanya ili tumpokee Yesu akirudi?
Yesu alikuja
Yesu yupo
Yesu atakuja tena.
Nakutakia Jumatano njema
Heri Buberwa Nteboya