Date: 
02-12-2024
Reading: 
Ufunuo wa Yohana 3:1-16

Hii ni Advent;

Jumatatu asubuhi tarehe 02.12.2024

Ufunuo wa Yohana 3:1-6

[1]Na kwa malaika wa kanisa lililoko Sardi andika; 

Haya ndiyo anenayo yeye aliye na hizo Roho saba za Mungu, na zile nyota saba. Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa hai, nawe umekufa.

[2]Uwe mwenye kukesha, ukayaimarishe mambo yaliyosalia, yanayotaka kufa. Maana sikuona matendo yako kuwa yametimilika mbele za Mungu wangu.

[3]Basi kumbuka jinsi ulivyopokea, na jinsi ulivyosikia; yashike hayo na kutubu. Walakini usipokesha, nitakuja kama mwivi, wala hutaijua saa nitakayokuja kwako.

[4]Lakini unayo majina machache katika Sardi, watu wasioyatia mavazi yao uchafu. Nao watakwenda pamoja nami hali wamevaa mavazi meupe, kwa kuwa wamestahili.

[5]Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake.

[6]Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.

Bwana analijia Kanisa lake;

Neno Ufunuo ni tafsiri ya Kigiriki "apokalupsis" na maana yake ni "Ufunuo" au "ufichuo"

Kitabu hiki huitwa Ufunuo kwa sababu kinatoa ujumbe kwa njia ya maono, yaliyofunuliwa na Mungu mwenyewe ili kueleza mapenzi yake na siri za mbinguni.

Hayo yote, ni pamoja na somo letu la Leo asubuhi, kama tulivyolisoma hapo juu.

Tunakumbushwa kutafakari juu ya unyenyekevu, kwamba tukiwa wanyenyekevu Mungu atatuinua.

Asubuhi hii tunaona nini?

Kanisa linaweza kuonekana lipo, lakini likawa limekufa. Hii ndiyo ilikuwa hali ya Kanisa la Sardi, lililokuwa karibu maili 50 mashariki mwa Efeso. Baada ya karne 20, tatizo hili yawezekana likawepo.;

Sasa basi; 

1.Tunashuhudia ukweli?

Kama lilivyo Kanisa la Sardi, Yesu hatutafakarishi nje ya hapa. Kanisa lilikuwa na nguvu, na lilionekana kukua kiroho. Lakini Kristo aliliona Kanisa hili lililokufa kiroho. Walikiwepo wachache waliokuwa wenye haki, lakini Yesu hakuwa na muono wa Kanisa kwa ujumla wake.

Wakati mwingine, kifo cha kiroho kinaweza kuwepo kanisani bila kuonekana kwa macho ya kawaida. Mahudhurio yanaweza kuwa mazuri, matoleo yaweza kuwa makubwa sana, shughuli za diakonia nyingi sana, na watu kuonekana hai. Yote haya yakiwepo, kujikweza kiroho kunaweza kuanza kutawala. Maisha ya toba ya kweli na msamaha yanaanza kupotea. Wengi wetu tunaweza kuwa tunasoma na kulifahamu neno, lakini kumbe ndo hatujui.

Kanisa linaweza kuwa hai kiroho, mahudhurio yakiwa mazuri, na shughuli nyingine zote zikiendelea. Hoja hapa sio kinachoendelea kwa nje, lakini mioyo ikoje?

Tuko wanyenyekevu katika utume huu? 

2.Tuamke, tuimarike.

Yesu aliliona Kanisa la Sardi limekufa. Analiambia kuamka na kuimarika. Pamoja na kwamba Kanisa lilikuwa katika hali mbaya kiasi cha kuonekana limekufa, Yesu bado alijua kuwa kanisa lipo.

Kanisa linatakiwa kuangalia nafasi yake kiroho, kila mmoja akichukua hatua ya toba, kwa unyenyekevu mkubwa. 

Mamilioni ya wakristo wanatumia muda mwingi kuwafuatilia wahubiri wakubwa sehemu tofauti tofauti mf kwenye Televisheni. na kusikiliza shuhuda tofauti tofauti ambazo zimekuwa kama tamaduni. Ni muhimu kujua dunia na tamaduni zake, lakini kuepuka falsafa zinazohatarisha nafasi yetu kiroho.

Mtafute Mungu lakini kwa msingi wa kuwa mnyenyekevu. 

3.Tukumbuke tulivyopokea na kutubu.

Yesu hakuliacha Kanisa bila mbadala wa njia sahihi ya kuishi. Suluhisho la kifo cha kiroho ni kukumbuka tulivyopokea, na kutubu. Yesu anatukumbusha kutubu, akisema tusipotubu hukumu inatujia. Tutubu wakati wote, maana hukumu ikija tutakuwa tumechelewa.

Ni wakati sasa wa kutubu na kuokolewa.

Tunayo ya kukumbuka.

Tunaweza kukumbuka yote tuliyofundishwa na uzoefu wetu katika maisha ya ukristo hai. Twaweza kukumbuka yote ambayo Yesu alifanya kwa ajili yetu. 

Tukitubu;

-Tunabadili maisha yetu

-Tunaondoa mawazo, maneno na matendo yanayotudumaza kiroho.

-Tunapata nguvu ya kudumu katika sala na neno la Mungu.

-Tunakua kiroho.

Tunapofanya toba, twende mbele za Mungu kwa unyenyekevu.

4.Tukimrudia Mungu atatupa thawabu.

Kanisa la Sardi lilikuwa na waamini waliokuwa wamemuacha Kristo. Walikwenda kanisani na kuishi kwa mazoea. Hawakujua kinachoendelea maana rohoni wamekufa. 

Tunahitaji kujitambua kama tumekufa au tu wazima, na kumwendea Bwana kwa unyenyekevu na toba ya kweli.

Tutubu na kunyenyekea ili tuurithi uzima wa milele.

Uwe na wiki njema, katika Majira haya ya Majilio

 

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650