Jumamosi asubuhi tarehe 16.11.2024
Isaya 66:13-18
13 Mfano wa mtu ambaye mama yake amfariji, ndivyo nitakavyowafariji ninyi; nanyi mtafarijiwa katika Yerusalemu.
14 Nanyi mtaona, na mioyo yenu itafurahi, na mifupa yenu itasitawi kama majani mabichi; na mkono wa Bwana utajulikana, uwaelekeao watumishi wake, naye atawaonea adui zake ghadhabu.
15 Maana Bwana atakuja na moto, na magari yake ya vita kama upepo wa kisulisuli; ili atoe malipo ya ghadhabu yake kwa moto uwakao, na maonyo yake kwa miali ya moto.
16 Kwa maana Bwana atateta na wote wenye mwili, kwa moto na kwa upanga wake; nao watakaouawa na Bwana watakuwa wengi.
17 Watu wale wajitakasao, na kujisafisha katika bustani, nyuma yake aliye katikati; wakila nyama ya nguruwe, na machukizo, na panya; watakoma pamoja, asema Bwana.
18 Nami nayajua matendo yao na mawazo yao; wakati unakuja nitakapokusanya mataifa yote na lugha zote; nao watakuja, nao watauona utukufu wangu.
Mwenye kuvumilia hata mwisho ndiye atakayeokoka;
Sehemu hii ya mwisho ya kitabu cha Nabii Isaya ni ujumbe wa faraja kwa Israeli wakiwa wamerejea kutoka uhamishoni. Bwana anawaahidi kuwa faraja yao daima. Anawahakikishia furaha ya mioyo yao na ustawi wa roho zao wakimtegemea. Bwana anaendelea kuahidi kuwaangamiza wote ambao watakuwa kikwazo kwa Taifa lake. Bwana anatoa ole kwa watendao uovu, akiwataka Taifa lake kuwa wachaji daima.
Tumeona faraja ya Mungu kwa Israeli baada ya kutoka uhamishoni. Sisi tunayo faraja ya Kristo inayodumu mioyoni mwetu, maana yeye ndiye hutuongoza na kutuondolea shida zote. Suluhisho la kudumu kwetu ni kudumu katika Kristo atupaye faraja ya kweli kuelekea uzima wa milele. Amina
Jumamosi njema
Heri Buberwa