Jumatatu asubuhi tarehe 11.11.2024
2 Wathesalonike 2:1-5
1 Basi, ndugu, tunakusihini, kwa habari ya kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, na kukusanyika kwetu mbele zake,
2 kwamba msifadhaishwe upesi hata kuiacha nia yenu, wala msisitushwe, kwa roho, wala kwa neno, wala kwa waraka unaodhaniwa kuwa ni wetu, kana kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwapo.
3 Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uharibifu;
4 yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.
5 Je! Hamkumbuki ya kuwa wakati nilipokuwapo pamoja nanyi naliwaambieni hayo?
Mwenye kuvumilia hata mwisho ndiye atakayeokoka;
Mtume Paulo anawaandikia watu wa Kanisa la Thesalonike kuhusu kutoiacha imani yao. Anawata kukaa katika imani ili Bwana atakaporudi awakute katika imani kama walivyompokea. Anawasisitiza kutodanganywa kwa njia yoyote kumuacha Kristo aliye Mwokozi wao, yaani wasimamie imani waliyonayo.
Ujumbe huu wa Paulo unatujia leo asubuhi ukitutaka kutofadhaishwa na mafundisho ya ajabu hata kumuacha Yesu. Tukatae kudanganywa na wale wahubirio Injili kwa malengo yao binafsi. Tunawafahamu kwa sababu hawahubiri neema ya Mungu, kwa njia ya Yesu aliyekufa msalabani. Tusidanganyike, maana mwenye kuvumilia hata mwisho ndiye atakayeokoka. Amina
Uwe na wiki njema
Heri Buberwa