Date: 
31-10-2024
Reading: 
Habakuki 2:1-4

Alhamisi asubuhi tarehe 31.10.2024

Habakuki 2:1-4

[1]Mimi nitasimama katika zamu yangu, nitajiweka juu ya mnara, nitaangalia ili nione atakaloniambia, na jinsi nitakavyojibu katika habari ya kulalamika kwangu.

[2]BWANA akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji.

[3]Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia.

[4]Tazama, roho yake hujivuna, haina unyofu ndani yake; lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake.

Mwenye haki ataishi kwa Imani;

Utangulizi;

Kuhusu kitabu cha Habakuki;

Ufalme wa Israeli Kaskazini uliangukia mikononi mwa Ashuru mwaka 722KK, ufalme wa kusini, yaani Yuda ukiachwa katika nchi ya ahadi. Mwaka 612 KK Babeli ilikuwa tishio kwa Ashuru, kwa kuitawala. Sasa ikawa Babeli imekuwa tishio kwa kuivamia Yuda. Mbaya zaidi, mfalme Yosia pamoja na kuanza matengenezo mwaka 621KK, bado alipoteza ushawishi, na Yuda ikashuka kiroho (1:2-4). Hapa ndipo alikuja Nabii Habakuki akiwaandikia watu Mungu aliyomfundisha kuhusu kuja kwake, hukumu ya wote, yaani Yuda na Babeli, nguvu yake juu ya mwanadamu na upendo wake uliojaa uaminifu. 

Kitabu hiki kinazungumzia suala la mateso, dhambi na haki ya Mungu. Habakuki anaanza kwa kumlalamikia Mungu kuwa Yuda hakutekeleza ujumbe aliopewa. Anauliza; ni lini Yuda waendelee katika uovu bila kuadhibiwa? Mungu anajibu kuwa anaandaa adhabu itakayotolewa kwa kutumia Wakaldayo (Wababeli). Habakuki anaukataa mpango huo akisema kama Mungu ni Mtakatifu na wa haki, na Wayahudi ni watu wake, itawezekanaje Wakaldayo wenye maovu mengi kuliko Yuda watumiwe na Mungu? Mungu anajibu kuwa kila dhambi huleta hukumu. Hivyo wote watahukumiwa kwa uovu wao, kama tutakavyoona mbeleni.

Mwandishi;

Mwandishi ni Habakuki ambaye alikuwa Mlawi, akiwa mwimbaji hekaluni (3:1,19)

Lini kitabu kiliandikwa?

Umaarufu wa Babeli katika Habakuki unaonekana kwa mwaka wa 612KK lakini Babeli ilikuwa haijaivamia Yuda, hivyo kupeleka dhana ya kuandikwa 605KK. Ingawa hakuna wafalme wanaotajwa, uhalisia wa taifa la Mungu kiroho kwa wakati ule unashawishi uandishi kuwa karibu na mwisho wa utawala wa Mfalme Yosia, au labda baada ya Yehoyakimu kuchukua nafasi yake mwaka 609KK 

(2Nyak 36:8, Yer 22:18-19)

Sifa ya pekee;

Habakuki ndicho kitabu pekee cha Agano la kale ambacho kwa sehemu kubwa kina mazungumzo kati ya Mungu na mwanadamu. Vingine ni kwa sehemu tu kama Yona, Ayubu na vingine vichache vyenye mazumgumzo kidogo. Vitabu vingine vyote vimejaa unabii na mafundisho kama manabii walivyokuwa wakitumwa.

Lengo la Habakuki kuandika kitabu hiki ilikuwa kutangaza kuwa Yuda wenye dhambi wataadhibiwa. Pia kutangaza kuwa japokuwa Babeli wangetumika kuwaadhibu Yuda, Babeli nao wangeadhibiwa. Ujumbe mwingine pia ulihusu Mungu kuwaacha Yuda walio watiifu (2:4)

Sasa tuingie kwenye somo;

Kanisa la Kilutheri linao umuhimu wa pekee na kitabu hiki, kupitia kwa Mtume Paulo ambaye aliwaandikia warumi kuwa "mwenye haki ataishi kwa imani.

Wengi tumesikia maneno haya toka kwa Martin Luther, lakini ukweli ni kuwa hata Mtume Paulo mwenyewe aliyatoa kwa Habakuki, japokuwa kwenye Agano la kale hayakupewa nafasi sana kwa sababu ya ufupi wa unabii wake. Tumeyasoma katika somo letu leo;

Habakuki 2:4

[4]Tazama, roho yake hujivuna, haina unyofu ndani yake; lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake.

Maneno haya yamenukuliwa mara tatu katika Agano jipya kama ifuatavyo;

Warumi 1:17

[17]Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani.

Wagalatia 3:11

[11]Ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani.

Waebrania 10:38

[38]Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; 

Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye.

"Katika injili ya Mtume Paulo kwa Warumi, maneno haya yanaifanya imani kuwa kitu cha muhimu na pekee, katika Wagalatia ni fundisho jinsi ya kuishi, na katika Waebrania ni msisitizo juu ya imani timilifu". Hadi hapo tunaona kuwa msingi wa kuishi kwetu ni imani katika Kristo, na hapo ndipo tunahesabiwa haki. 

Uhusiano wetu na Habakuki;

Nabii Habakuki ni nabii wa zama hizi, ambaye aliishi kama sisi, akijiuliza ni kwa nini Mungu aliruhusu baadhi ya mambo kutokea? Habakuki aliishi wakati rushwa imeshamiri, mgawanyiko ukiwa mkubwa kwenye jamii. Kazi za shetani zilikuwa wazi, na maadili kushuka. Nabii huyu aliona haya na ndio akaja na unabii (1:2-4)

Habakuki anakiri kumlilia Bwana na hasikii jibu! Hili ni tatizo kubwa, yaani sala isiyojibiwa. Ni mtu aliyesumbuka kwa sababu ya nchi yake, akiona kila kitu hakiko sawa. Wakati ambao haki haikutendeka hata kidogo. Habakuki alisumbuka maana sala yake haikujibiwa. Ndio maana anamlilia BWANA;

Habakuki 1:2

[2]Ee BWANA, nilie hata lini, wewe usitake kusikia? Nakulilia kwa sababu ya udhalimu, ila hutaki kuokoa.

Inapotokea sala yako haijibiwi unafanyaje? Katikati ya jamii iliyojaa uovu? Zidi kuwa mwenye imani katika maisha yako, BWANA hatakuacha. 

Alisubiri jibu;

Somo la leo ni Habakuki akisubiri jibu la sala yake. Alichagua kusubiri jibu. Yapo makanisa/walimu/wahubiri leo ambayo(o) yanaendesha mahubiri/mafundisho juu ya kuomba, kwamba kwa kuomba watakuwa watu wa tofauti duniani hapa. Ni vyema kabisa. Lakini hawatoi maelekezo nini cha kufanya Mungu asipojibu!

 Mungu hakumjibu Habakuki moja kwa moja kama alivyotegemea, bali alimuahidi kuona matendo yake. Aliahidi kuwaangamiza wasio haki, Babeli kuivamia Yuda.

Huu ndiyo ujumbe wa Bwana leo, kuwa matendo ya uovu mwisho wake ni kuangamia. Bwana anamwambia Habakuki kuwa Yuda itapata hukumu stahiki. Hukumu hii ni kwa wote watendao uovu.

Mungu alijibu sala ya Habakuki kwa maelekezo ya matokeo ya mambo yaliyokuwepo. Kumbe Mungu hujibu kwa njia tofauti, akimpa hitaji lake aombaye, au kumwelekeza yampasayo kufanya, au kuonesha mwisho unaofaa.

Matengenezo ya Kanisa;

Kama tulivyoona, Habakuki aliishi wakati rushwa imeshamiri, mgawanyiko ukiwa mkubwa kwenye jamii, uonevu na kutotenda haki. 

Hii ni sawa na Martin Luther aliyeishi wakati ambao Kanisa liliacha msingi wake ambao ni neno la Mungu. Haki ilipotea miongoni mwa wengi, imani ikaanza kuonekana jambo la kawaida. Kama Habakuki, Mungu akamtumia Luther kufanya Matengenezo ya Kanisa, kwa kuangaza uovu uliokuwa ukiendelea Kanisani. Alisimamia ukweli wa neno na Mungu, na haki itokayo kwake. Alihubiri ukuu wa Mungu usiofananishwa, neno lake, msamaha wa dhambi, imani ya kweli, na utukufu wa Mungu usio na ubia. Kumbe ujumbe wa Martin Luther ulikuwa mwendelezo wa unabii wa Habakuki! Kuwa hukumu ya Mungu ipo, ni muhimu kusimama katika kweli.

Tunaposoma kuhusu Habakuki, ni miaka takribani 600KK. Martin Luther aliweka wazi fikra za matengenezo ya Kanisa mwaka 1517BK. Kutoka kwa Habakuki hadi hapo kwa Luther ni miaka zaidi ya 2000, na hadi leo ni karibu miaka zaidi ya 2600. Habakuki hakuona, aliambiwa "ufalme wa Mungu utakuja". Ujumbe huu unadumu hadi leo, kuwa "ufalme wake utakuja".

Leo hii sisi tuliokusanyika tunapewa ujumbe huu, kuwa "ufalme wa Mungu utakuja". Lini? Tuendelee kusubiri. Hatuwezi kujua ni lini, japokuwa wapo waliojifanya manabii wakatabiri (japo hawajatabiri watakufa lini). La muhimu imani yetu iwe kwa Mungu, tukingojea ahadi yake. 

Martin Luther alisema;

"Imani ni maisha, yenye kuamini katika neema ya Mungu, kwamba mtu anaweza akaishi katika imani hiyo"

Aliongeza; "Imani hutufanya wapya"

Baada ya Habakuki na manabii wengine, Yesu alikuja kuleta ujumbe wa imani kwa Mungu, kama msingi wa wokovu kwa mwanadamu. Ni mara nyingi aliponya na kusema "Imani yako imekuponya". Kumbe hatuwezi kumwendea Bwana pasipo imani ya kweli.

Pamoja na yote tuonayo yanaendelea lakini hayako sawa, sisi tunaitwa kuwa wenye haki kwa njia ya imani, tukijua upo mwisho ambapo Yesu atarudi kwa hukumu. 

Kama alivyowahi kusema Martin Luther;

"Dhamira yangu imefungwa na neno la Mungu". Wewe dhamira yako imefungwa na nini? Fanya matengenezo ya maisha yako, Yesu anakuja. Ujumbe wa Habakuki ni BWANA Mungu siyo Mungu wa Israeli na Yuda tu, yeye ni Mungu wa ulimwengu wote. Yuda na Ukaldayo (Babeli) wataadhibiwa kwa kufuata maovu yao. Vivyo hivyo, sisi nasi tutahukumiwa kadri ya matendo yetu. Tukimtegemea Mungu, tukawa waadilifu, hatuna haja ya kuogopa hukumu maana "Mwenye haki ataishi kwa imani" na Mungu atampa ushindi.

 

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650

bernardina.nyamichwo@gmail.com