Jumatano asubuhi tarehe 09.10.2024
Matendo ya Mitume 3:11-16
11 Basi alipokuwa akiwashika Petro na Yohana, watu wote wakawakusanyikia mbio katika tao lile lililoitwa tao la Sulemani, wakishangaa sana.
12 Hata Petro alipoyaona haya akawajibu wale watu, Enyi Waisraeli, mbona mnastaajabia haya, au mbona mnatukazia macho sisi, kana kwamba tumemfanya huyu aende kwa nguvu zetu sisi, au kwa utauwa wetu sisi?
13 Mungu wa Ibrahimu na wa Isaka na wa Yakobo, Mungu wa baba zetu, amemtukuza mtumishi wake Yesu, ambaye ninyi mlimsaliti na kumkana mbele ya Pilato, alipokuwa ametoa hukumu yake afunguliwe.
14 Bali ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji;
15 mkamwua yule Mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake.
16 Na kwa imani katika jina lake, jina lake limemtia nguvu mtu huyu mnayemwona na kumjua; na imani ile iliyo kwake yeye imempatia huyu uzima huu mkamilifu mbele yenu ninyi nyote.
Nguvu ya Imani katika Yesu Kristo;
Mistari kumi ya kwanza ya sura ya tatu ya Matendo ya Mitume inaonesha Petro na Yohana wakiingia hekaluni kusali, mlangoni wanakutana na kiwete aliyekuwa akiomba kupata kitu kwao. Kwa matarajio ya kupata chochote, Petro anamuombea anatembea katika jina la Yesu! Kiwete aliyetegemea labda fedha pale mlangoni anapata kutembea!
Sasa ndipo linakuja somo la leo asubuhi, aliyekuwa kiwete anaonekana akitembea, watu wanastaajabu. Inakuwa habari kubwa! Petro anawaambia watu wasishangae, kwamba uponyaji umewezekana kwa jina la Yesu ambaye walimkataa, wakamsulibisha na kumuua. Petro anawaambia kwamba Yesu alifufuka, na imani katika yeye ndiyo hutenda haya (yaani uponyaji). Tusiiache Imani katika KristoYesu. Amina
Jumatano njema
Heri Buberwa
Mlutheri