Date: 
07-10-2024
Reading: 
Luka 5:1-11

Jumatatu asubuhi tarehe 07.10.2024

Luka 5:1-11

1 Ikawa makutano walipomsonga wakilisikiliza neno la Mungu, yeye alikuwa amesimama kando ya ziwa la Genesareti,

2 akaona vyombo viwili vimekaa kando ya ziwa, lakini wavuvi wametoka, wanaosha nyavu zao.

3 Akaingia katika chombo kimoja, ndicho chakeSimoni, akamtaka akipeleke mbali kidogo na pwani. Akaketi, akawafundisha makutano ali chomboni.

4 Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki.

5 Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.

6 Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika;

7 wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama.

8 Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana.

9 Maana alishikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi wa samaki walioupata;

10 na kadhalika Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika wa Simoni. Yesu akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu.

11 Hata walipokwisha kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata.

Nguvu ya imani katika Yesu Kristo;

Yesu anafuatwa na makutano akiwafundisha, umati ulikuwa mkubwa hadi hadi akamtaka Simoni apeleke chombo mbali na pwani. Baada ya kuwa amefundisha, akamwambia Simoni kushusha nyavu ili wakavue samaki. Walikuwa wamevua usiku kucha wasipate kitu, lakini walipotii maelekezo ya Yesu wakashusha nyavu na kupata samaki wengi. Samaki walikuwa wengi hadi wakaomba msaada wa kuwatoa ziwani.

Tunaona imani ya wanafunzi wa Yesu katika somo la asubuhi hii. Haikuwa rahisi kupata samaki asubuhi, lakini kwa neno la Bwana walipata samaki wengi. Walikuwa na imani katika Yesu, wakavua na kupata samaki asubuhi. Lakini pia katika mstari wa 11 tunaona wale wavuvi wanaacha kazi yao na vifaa vyao kumfuata Yesu. Walimtii Yesu aliyewaita, wakamwamini na kumfuata. Mwamini Yesu uokolewe. Amina

Uwe na Jumatatu njema

Heri Buberwa Nteboya