Date: 
05-10-2024
Reading: 
Kumbukumbu la Torati 31:9-13

Jumamosi asubuhi tarehe 05.10.2024

Kumbukumbu la Torati 31:9-13

9 Musa akaiandika torati hii, akawapa makuhani, wana wa Lawi, waliolichukua sanduku la agano la Bwana, na wazee wote wa Israeli.

10 Musa, akawaamuru, akasema, Mwisho wa kila mwaka wa saba, wakati wa maachilio, wakati ulioamriwa wa sikukuu ya vibanda,

11 Israeli wote wafikapo ili kuonekana mbele za Bwana, Mungu wako, mahali pale atakapopachagua, uisome torati hii mbele ya Israeli wote masikioni mwao.

12 Wakusanye watu, wanaume na wanawake na watoto, na mgeni wako aliyemo malangoni mwako wapate kusikia na kujifunza, na kumcha Bwana, Mungu wenu, na kuangalia kutenda maneno yote ya torati hii;

13 na watoto wao wasiojua, wapate kusikia na kujifunza kumcha Bwana, Mungu wenu, siku zote mtakazokaa katika nchi mnayoivukia Yordani ili kuimiliki.

Tuwajali watoto wetu katika Bwana;

Musa alielekezwa na Mungu kuweka pamoja Torati na kuwapa Israeli. Musa anaelekeza kama alivyoagizwa na Bwana, kuwa Torati isomwe mbele ya Israeli wote masikioni mwao mahali pale atakapopachagua Bwana mwisho wa kila mwaka wa saba, wakati wa maachilio, wakati ulioamriwa wa sikukuu ya vibanda. Inaelekezwa kwamba Torati inaposomwa asibaki mtu hata mmoja, wahudhurie wote wanaume, wanawake na watoto. 

Kwa mtazamo wa Kiinjili, somo la asubuhi ya leo ni kwetu waamini kumwamini Yesu na kulishika neno lake. Waamini wote wanaume, wanawake na watoto tunaitwa kumcha Bwana kwa njia ya neno lake. Tumwamini Yesu maana yeye ndiye ukamilifu wa Torati. Mstari wa 13 unasisitiza watoto kusikia na kujifunza kumcha Bwana. Tuwafundishe watoto kumjua Yesu Kristo, ili jamii iwe na kizazi kinachomcha Bwana. Amina

Heri Buberwa 

Mlutheri