Alhamisi asubuhi tarehe 03.10.2024
Kumbukumbu la Torati 6:20-25
[20]Na zamani zijazo atakapokuuliza mwanao, akikuambia, N’nini mashuhudizo, na amri, na hukumu, alizowaagiza BWANA, Mungu wetu?
[21]Ndipo umwambie mwanao, Tulikuwa watumwa wa Farao huko Misri; BWANA, akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu;
[22]BWANA akaonya ishara na maajabu, makubwa, mazito, juu ya Misri, na juu ya Farao, na juu ya nyumba yake yote, mbele ya macho yetu;
[23]akatutoa huko ili kututia huku, apate kutupa nchi aliyowaapia baba zetu.
[24]BWANA akatuamuru kuzifanya amri hizi zote, tumche BWANA, Mungu wetu, tuone mema sikuzote ili atuhifadhi hai kama hivi leo.
[25]Tena itakuwa haki kwetu, tukitunza kufanya maagizo haya yote mbele ya BWANA, Mungu wetu, kama alivyotuagiza.
Tuwajali watoto wetu katika Bwana;
Israeli wanaagizwa kuwafundisha watoto wao juu ya nguvu ya Mungu kwao, na upendo wake, kwa jinsi alivyowaokoa toka utumwani. Bwana anawataka Israeli kuwafundisha watoto wao juu ya amri zake, ili wazidi katika kumwamini na kumtumikia yeye.
Ndivyo Mungu anavyotutaka kufundisha na kuhubiri kwa watu wote juu ya nguvu yake na wokovu wake, ya kuwa yeye ndiye mkombozi wa ulimwengu. Anatutaka kuhubiri kuwa, yeye ndiye BWANA aokoaye, anayestahili kuabudiwa na ulimwengu wote.
Ni wajibu wetu kuhubiri habari njema ya wokovu kwa watu wote, ili imani hii ya kweli katika Yesu Kristo idumu na kukua, Kanisa lake likikua na kuongezeka katika kuueneza ufalme wake ili watu wote waokolewe na kumtumikia yeye. Amina.
Siku njema
Heri Buberwa