Jumanne asubuhi tarehe 24.09.2024
Yeremia 18:5-12
5 Ndipo neno la Bwana likanijia, kusema,
6 Ee nyumba ya Israeli, je! Siwezi mimi kuwatendea ninyi vile vile kama mfinyanzi huyu alivyotenda? Asema Bwana. Angalieni, kama udongo ulivyo katika mkono wa mfinyanzi, ndivyo mlivyo ninyi katika mkono wangu, Ee nyumba ya Israeli.
7 Wakati wo wote nitakapotoa habari za taifa, na habari za ufalme, kuung'oa, na kuuvunja, na kuuangamiza;
8 ikiwa taifa lile nililolitaja litageuka, na kuacha maovu yake nitaghairi, nisitende mabaya yale niliyoazimia kuwatenda.
9 Na wakati wo wote nitakapotoa habari za taifa, na habari za ufalme, kuujenga na kuupanda,
10 ikiwa watatenda maovu mbele za macho yangu, wasiitii sauti yangu, basi nitaghairi, nisitende mema yale niliyoazimia kuwatendea.
11 Haya! Basi, ukawaambie watu wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, ukisema, Bwana asema hivi, Tazama, ninafinyanga mabaya juu yenu, na kuwaza mawazo juu yenu; rudini sasa, kila mmoja na aiache njia yake mbaya; zitengenezeni njia zenu, na matendo yenu.
12 Lakini wao wasema, Hapana tumaini lo lote; maana sisi tutafuata mawazo yetu wenyewe, nasi tutatenda kila mmoja wetu kwa kuufuata ushupavu wa moyo wake mbaya.
Uchaguzi wako ndiyo maisha yako;
Yeremia anawasihi Taifa la Mungu kuupokea ujumbe wa Bwana kama alivyokuwa ametumwa kwao. Yeremia anaonesha kwamba ujumbe wa Bwana ndiyo uliobeba hatma ya Taifa lake, hivyo walitakiwa kumsikiliza Bwana kwa ajili ya hatma yao. Ni kwa njia ya kuusikia ujumbe wa kinabii wangeweza kujua jinsi ya kumfuata Bwana na hatma yao.
Ujumbe tunaoupata ni kuisikia sauti ya Mungu katika maisha yetu. Yaani tuchague kumwamini na kumshika Yesu atuongozaye na kutufundisha jinsi ya kuenenda katika maisha yetu. Tuchague kumwamini na kumsikia Yesu maana ni kwa njia ya neno lake tutaurithi uzima wa milele. Mchague Yesu daima. Amina.
Jumanne njema
Heri Buberwa