Date: 
20-09-2024
Reading: 
Matendo 15:23-29

Ijumaa asubuhi tarehe 20.09.2024

Matendo ya Mitume 15:23-29

23 Mitume na ndugu wazee, kwa ndugu zetu walioko Antiokia na Shamu na Kilikia, walio wa Mataifa; Salamu.

24 Kwa kuwa tumesikia ya kwamba watu waliotoka kwetu wamewasumbua kwa maneno yao, wakipotosha roho zenu, ambao sisi hatukuwaagiza;

25 sisi tumeona vema, hali tumepatana kwa moyo mmoja, kuwachagua watu na kuwapeleka kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo,

26 watu waliohatirisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo.

27 Basi tumewatuma Yuda na Sila, watakaowaambia wenyewe maneno yayo hayo kwa vinywa vyao.

28 Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima,

29 yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya vema. Wasalamu.

Uhuru wetu katika Kristo Yesu;

Paulo alikuwa amewaongoza Mitume wenzake kuhubiri habari za Yesu mbele ya baraza la Yerusalemu. Baraza ambalo lilikuwa na baadhi ya waumini wa torati, lakini Paulo na wenzake walilitetea jina la Yesu katika mazingira magumu (15:1-21). Mitume walikuwa na wakati mgumu mbele ya baraza, lakini hawakutetereka.

Soma kwa sehemu;

Matendo ya Mitume 15:4-7

4 Walipofika Yerusalemu wakakaribishwa na kanisa na mitume na wazee, nao wakawaeleza mambo yote Mungu aliyoyafanya pamoja nao.
5 Lakini baadhi ya madhehebu ya Mafarisayo walioamini wakasimama wakisema, Ni lazima kuwatahiri na kuwaagiza kuishika torati ya Musa.
6 Mitume na wazee wakakusanyika wapate kulifikiri neno hilo.
7 Na baada ya hoja nyingi Petro akasimama, akawaambia, Ndugu zangu, ninyi mnajua ya kuwa tangu siku za kwanza Mungu alichagua miongoni mwenu ya kwamba Mataifa walisikie neno la Injili kwa kinywa changu, na kuliamini.

Sasa baada ya Injili ya kueleweka iliyosimama katika kumtetea Yesu, Wazee wa baraza na Mitume wakapatana kupeleka ujumbe wa Kristo Antiokia. Ndiyo ujumbe tuliousoma leo asubuhi (soma tena hapo juu). 

Wanawataka watu wa Antiokia wasisumbuke na mafundisho ya kupotosha. Wanawasihi kuwasikiliza wajumbe waliotumwa kwao kupeleka habari za Yesu Kristo. Wanawasihi zaidi kuacha mambo ya kale na kuushika ujumbe wa Kristo. Tumshike Yesu Kristo aliyetuweka huru. Amina.

Ijumaa njema

Heri Buberwa