Date: 
19-09-2024
Reading: 
Wakolosai 2:8-18

Alhamisi asubuhi tarehe 19.09.2024

Wakolosai 2:8-17

8 Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo.

9 Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili.

10 Na ninyi mmetimilika katika yeye aliye kichwa cha enzi yote na mamlaka.

11 Katika yeye mmetahiriwa kwa tohara isiyofanyika kwa mikono, kwa kuuvua mwili wa nyama, kwa tohara ya Kristo.

12 Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu.

13 Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote;

14 akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani;

15 akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.

16 Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato;

17 mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.

Uhuru wetu katika Kristo Yesu;

Mtume Paulo anaonya juu ya elimu ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu wala si kwa jinsi ya Kristo. Paulo anasema kuwa utimilifu wote uko katika Kristo ambaye tulizikwa pamoja naye katika ubatizo, na katika huo tukafufuliwa naye katika ubatizo. Kwa maelezo ya Paulo, hukumu juu ya sheria imefutwa. Ndiyo maana Paulo anasema tusihukumiwe kwa vyakula, vinywaji, mwandamo wa mwezi, sabato n.k

Maisha yetu yamtazame Kristo, na siyo sheria maana Kristo ndiye utimilifu wa hiyo sheria. Tusihukumiwe kwa sababu ya aina za maisha kwa sababu tu hatujaifuata sheria, maana sisi tuko huru katika Yesu Kristo aliyekufa msalabani kwa ajili yetu. Msaada wetu ni katika jina la Bwana aliyeziumba mbingu na nchi. Amina

Alhamisi njema

Heri Buberwa