Date: 
18-09-2024
Reading: 
Mathayo 12:9-14

Jumatano asubuhi tarehe 18.09.2024

Mathayo 12:9-14

9 Akaondoka huko, akaingia katika sinagogi lao.

10 Na tazama, yumo mtu mwenye mkono umepooza; wakamwuliza, wakisema, Ni halali kuponya watu siku ya sabato? Wapate kumshitaki.

11 Akawaambia, Ni mtu yupi miongoni mwenu mwenye kondoo mmoja, na yule kondoo ametumbukia shimoni siku ya sabato, asiyemshika akamwopoa?

12 Je! Mtu ni bora kuliko kondoo mara ngapi? Basi ni halali kutenda mema siku ya sabato.

13 Kisha akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako; akaunyosha, ukapona, ukawa mzima kama wa pili.

14 Lakini wale Mafarisayo wakatoka wakafanya shauri juu yake jinsi ya kumwangamiza.

Uhuru wetu katika Kristo Yesu;

Yesu aliingia katika sinagogi ikiwa ni sabato akamkuta mtu aliyepooza mkono. Huenda Mafarisayo walihisi ambacho Yesu angefanya, yaani kumponya aliyepooza. Wakamuuliza kama ni halali kuponya siku ya sabato. Yesu akawauliza kama wangekuwa tayari kumuacha kondoo atumbukie shimoni na kupotea kwa sababu ni sabato. Haionekani Mafarisayo wakimjibu Yesu, lakini Yesu alifanya uponyaji huku Mafarisayo wakiondoka na nia ya kumshtaki.

Mafarisayo walitawaliwa na sheria, kwamba siku ya sabato, usifanye kazi yoyote. Waliitii amri hii;

Kutoka 20:8-11

8 Ikumbuke siku ya Sabato uitakase.
9 Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote;
10 lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako.
11 Maana, kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo Bwana akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa.

Lakini Yesu aliye utimilifu wa torati anawafundisha kuwa wokovu ni kwa kila mtu, popote, wakati wowote. Kazi ya kuokoa ni ya Mungu, ni neema, siyo sheria. Hivyo sheria hiyo haina nafasi mbele ya wokovu wa mwanadamu, maana mwanadamu aliyeumbwa kwa mfano wa Mungu ni muhimu kuliko hiyo sheria na sabato. Tusifungwe na sabato, Kristo ametuweka huru. Amina.

Jumatano njema

Heri Buberwa