Date:
03-09-2024
Reading:
Matendo ya Mitume 11:27-30
Jumanne asubuhi tarehe 03.09.2024
Matendo ya Mitume 11:27-30
27 Siku zizo hizo manabii walitelemka kutoka Yerusalemu hata Antiokia.
28 Na tulipokusanyika akasimama mmoja wao, jina lake Agabo, akaonyesha kwa uweza wa Roho Mtakatifu kwamba njaa kubwa itakuja karibu katika dunia nzima, nayo ikatukia katika siku za Klaudio.
29 Na wale wanafunzi, kila mtu kwa kadiri ya alivyofanikiwa, wakaazimu kupeleka msaada kwa ndugu zao waliokaa Uyahudi.
30 Wakafanya hivyo, wakawapelekea wazee kwa mikono ya Barnaba na Sauli.
Mpende jirani yako;
Kanisa la Antiokia wakati wa Mitume lilikuwa na waamini wengi waliotawanyika kwa sababu ya dhiki iliyosababishwa na habari ya Stefano. Lakini pia watu wa Kipro na Kirene waliingia Antiokia, idadi ya waaminio ikawa kubwa. Habari zikafika masikioni mwa Kanisa la Yerusalemu, wakamtuma Barnaba aende huko Antiokia. Alipofika alifurahi kuona neema ya Mungu juu ya Kanisa la Antiokia.
Sasa somo la asubuhi hii ndipo linaonesha watu wa Kanisa la Yerusalemu wakishuka Antiokia. Mmoja kati yao akafunuliwa kuwa kungekuwa na njaa katika dunia nzima, na kweli ilitokea katika siku za Klaudio. Basi wale Mitume wakaazimia kupeleka msaada kwa ndugu wote ili wasife njaa.
Mitume hawakuishia kuhubiri Injili, waliwapa watu chakula. Huu ni upendo wa kweli kwa jirani. Nawe mpende Jirani yako kama nafsi yako. Amina
Jumanne njema
Heri Buberwa