Date: 
29-08-2024
Reading: 
Zaburi 52:1-9

Alhamisi asubuhi tarehe 29.08.2024

Zaburi 52:1-9

1 Kwa nini kujisifia uovu, Ewe jabari? Wema wa Mungu upo sikuzote.

2 Ulimi wako watunga madhara, Kama wembe mkali, Ewe mwenye hila

3 Umependa mabaya kuliko mema, Na uongo kuliko kusema kweli.

4 Umependa maneno yote ya kupoteza watu, Ewe ulimi wenye hila.

5 Lakini Mungu atakuharibu hata milele; Atakuondolea mbali; Atakunyakua hemani mwako; Atakung'oa katika nchi ya walio hai.

6 Nao wenye haki wataona; Wataingiwa na hofu na kumcheka;

7 Kumbe! Huyu ndiye mtu yule, Asiyemfanya Mungu kuwa nguvu zake. Aliutumainia wingi wa mali zake, Na kujifanya hodari kwa madhara yake.

8 Bali mimi ni kama mzeituni Umeao katika nyumba ya Mungu. Nazitumainia fadhili za Mungu milele na milele.

9 Nitakushukuru milele kwa maana umetenda; Nitalingojea jina lako kwa kuwa ni jema; Mbele ya wacha Mungu wako.

Kinywa cha mtu hunena yatokayo moyoni;

Zaburi hii ni matokeo ya Doegi, aliyekuwa upande wa Sauli katika kutaka kumuangamiza Sauli. Doegi allikuwa anamripoti Daudi kwa Sauli. Kumbuka Daudi alikuwa amepakwa mafuta kuwa mfalme, baada ya Sauli kukataliwa. Sauli alikuwa ameamuru makuhani kuteswa lakini wasaidizi wake walikataa, Doegi akakubali ambaye aliwachinja makuhani themanini na watano na wengine wengi wasio na hatia (1 Samweli 22:17-19). Ni kwa msingi huo Daudi anamuita Doegi muovu, muuaji ambaye ataangamizwa na Bwana kwa sababu ya ukatili wake (Zab 52:1-4)

Daudi anaamini kuwa Mungu ataulipiza uovu wa Doegi. Anaamini kuwa Mungu atauondolea mbali uovu wa Doegi na kumuangamiza (5-7). 

Daudi anategemea baraka ya Bwana, wakati Doegi ataharibiwa. Daudi anaonesha kusudi la Mungu. Maandiko hayaoneshi mwisho wa Doegi, ila la muhimu kujua hapa ni kuwa tuzae matunda mema maana hukumu haiepukiki. Amina

Alhamisi njema

 

Heri Buberwa