Jumatano asubuhi tarehe 28.08.2024
Matendo ya Mitume 8:18-24
18 Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema,
19 Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu.
20 Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali.
21 Huna fungu wala huna sehemu katika jambo hili, kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu.
22 Basi, tubia uovu wako huu, ukamwombe Bwana, ili kama yamkini, usamehewe fikira hii ya moyo wako.
23 Kwa maana nakuona u katika uchungu kama nyongo, na tena u katika kifungo cha uovu.
24 Simoni akajibu, akasema, Niombeeni ninyi kwa Bwana, yasinifikilie mambo haya mliyosema hata moja.
Kinywa cha mtu hunena yatokayo moyoni;
Mitume walikuwa katika kazi ya ya kuhubiri na kufundisha, waliombea wagonjwa na wenye shida. Kwa njia hii zilionekana ishara kadhaa miongoni mwa watu. Sasa Simoni alipoona haya, akawataka mitume wampe uwezo huo wa kuomba ili awape fedha! Huyu Simoni aliamini katika fedha. Lakini Petro alimwambia kuwa fedha yake na ipotelee mbali maana karama ya Mungu haipatikani kwa mali.
Petro alimwambia Simoni kwamba fedha zake hazikuwa na nafasi, na kwa maneno yake (Simoni) moyo wake haukuwa mnyofu mbele za Mungu. Maana yake hakunena vema mbele za Mungu. Petro anampa wito Simoni wa kutubu ili asamehewe kwa kufikiri kuwa karama ya Mungu inauzwa. Alikuwa katika kifungo cha uovu.
Simoni alielewa akaomba wamuombee kwa Bwana ili asikae katika kifungo cha uovu ambacho mwisho wake ungekuwa kufa dhambini. Simoni aliamini katika fedha. Fedha siyo mbaya, ni nzuri sana. Tena tuitafute kwa nguvu sana. Tuitafute fedha kwa njia halali, kwa utukufu wa Bwana. Ila tufahamu kwamba mbele za Mungu tunahitajika kuwaza, kunena na kutenda mema katika imani ya kweli ili tusikae katika kifungo cha uovu. Amina.
Jumatano njema.
Heri Buberwa