Date: 
24-08-2024
Reading: 
Zaburi 35:1-9

Jumamosi asubuhi tarehe 24.08.2024

Zaburi 35:1-9

1 Ee Bwana, utete nao wanaoteta nami, Upigane nao wanaopigana nami.

2 Uishike ngao na kigao, Usimame unisaidie.

3 Uutoe na mkuki uwapinge wanaonifuatia, Uiambie nafsi yangu, Mimi ni wokovu wako.

4 Waaibishwe, wafedheheshwe, Wanaoitafuta nafsi yangu. Warudishwe nyuma, wafadhaishwe, Wanaonizulia mabaya.

5 Wawe kama makapi mbele ya upepo, Malaika wa Bwana akiwaangusha chini.

6 Njia yao na iwe giza na utelezi, Malaika wa Bwana akiwafuatia.

7 Maana bila sababu wamenifichia wavu, Bila sababu wameichimbia shimo nafsi yangu.

8 Uharibifu na umpate kwa ghafula, Na wavu aliouficha umnase yeye mwenyewe; Kwa uharibifu aanguke ndani yake.

9 Na nafsi yangu itamfurahia Bwana, Na kuushangilia wokovu wake.

Nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari;

Katika Zaburi ya 35, Daudi anaomba Sala ya kukombolewa kutoka kwa adui. Anamuomba Bwana kupigana na wanaopigana naye. Anamuomba Bwana kusimama naye maana ndiye wokovu wake. Daudi anaomba waaibishwe, wafedheheshwe wanaoitafuta nafsi yake. Warudishwe nyuma wote wanaomzulia mabaya. Kwa ujumla Daudi anaomba Malaika wa Bwana kumshindia dhidi ya wanaopigana naye, na katika yote anasema nafsi yake itamfurahia Bwana na kuushangilia wokovu wake.

Baadhi yetu hutumia Zaburi hii kuwaombea wenzao mabaya. Sidhani kama ndiyo maana yake.

Daudi yeye alitaka Bwana kumlinda katika kazi aliyompa ya kuongoza watu wake katika Israeli, ilikuwa kazi ngumu, ambayo vita ilikuwa haiepukiki. Hivyo alikuwa anaomba dhidi ya adui zake.

Zaburi hii haituelekezi kuombea wengine mabaya, bali kuomba uongozi wa Mungu katika maisha yetu. Daudi aliomba Mungu amuepushe na mabaya, sisi tuombe Bwana asituache maishani. Yaani tumuige Daudi kuishi katika imani kwa Mungu, tukiomba bila kukoma. Tukimtegemea Yesu na kuomba daima hayo mengine yasiyofaa yataondoka yenyewe. Sisi tunafundishwa msamaha, na siyo kuombea watu mabaya. Tuwaombee wasiomjua Yesu wamwamini, na ulinzi wake uwe juu yetu daima. 

Daudi alikuwa mfalme, lakini alijua bila kumuomba Bwana adui zake wangemshinda. Alimwamini Bwana lakini pia alikuwa mnyenyekevu. Nasi bila Kristo hatuwezi kitu, hivyo tunyenyekee chini ya mkono wake ulio hodari. Amina

Jumamosi njema

 

Heri Buberwa