Date: 
22-08-2024
Reading: 
1Wafalme 21:27-29

Alhamisi asubuhi tarehe 22.08.2024

1 Wafalme 21:27-29

27 Ikawa, Ahabu alipoyasikia maneno hayo, akayararua mavazi yake, akavaa magunia mwilini mwake, akafunga, akajilaza juu ya magunia, akaenda kwa upole.

28 Neno la Bwana likaja kwa Eliya Mtishbi, kusema,

29 Huoni jinsi Ahabu alivyojidhili mbele yangu? Basi kwa sababu amejidhili mbele yangu, sitayaleta yale mabaya katika siku zake; ila katika siku za mwanawe nitayaleta mabaya hayo juu ya nyumba yake.

Nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari;

Ahabu Mfalme katika Israeli alikuwa katili sana. Alitawala kwa mabavu, aliua, alitesa watu. Haki haikuwepo kabisa. Eliya alitumwa na Bwana kumpelekea ujumbe kuwa Ahabu angeangamizwa na Bwana kwa sababu ya uongozi wake uliojaa ukatili. 

Soma kwa sehemu upate picha;

1 Wafalme 21:17-19

17 Neno la Bwana likamjia Eliya Mtishbi, kusema,
18 Ondoka, ushuke, ukutane na Ahabu mfalme wa Israeli, akaaye katika Samaria; yuko katika shamba la mizabibu la Nabothi, ndiko alikoshukia ili alitamalaki.
19 Ukamwambie, ukisema, Bwana asema hivi, Je! Umeua, ukatamalaki? Nawe utamwambia, kusema, Bwana asema hivi, Mahali pale mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba na damu yako, naam, damu yako.

Baada ya ujumbe wa Eliya kwa Ahabu kuwa naye angeangamizwa na Bwana, ndipo somo linaonesha Ahabu akirarua mavazi yake na kuvaa magunia akifanya toba. Na baada ya toba Bwana anasema hatayaleta mabaya katika siku zake Ahabu, ila kwa siku za mwanawe Ahabu. Yaani Mungu alimsamehe Ahabu baada ya kutubu. Ahabu alimwendea Mungu kwa unyenyekevu akasamehewa. Unyenyekevu hutuweka kwa Kristo daima. Amina

Alhamisi njema

Heri Buberwa