Date: 
17-08-2024
Reading: 
Yohana 6:60-65

Jumamosi asubuhi tarehe 17.08.2024

Yohana 6:60-65

60 Basi watu wengi miongoni mwa wanafunzi wake waliposikia, walisema, Neno hili ni gumu, ni nani awezaye kulisikia?

61 Naye Yesu akafahamu nafsini mwake ya kuwa wanafunzi wake wanalinung'unikia neno hilo, akawaambia, Je! Neno hili linawakwaza?

62 Itakuwaje basi, mmwonapo Mwana wa Adamu akipaa huko alikokuwako kwanza?

63 Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.

64 Lakini kuna wengine miongoni mwenu wasioamini. Kwa maana Yesu alijua tangu mwanzo ni nani wasioamini, naye ni nani atakayemsaliti.

65 Akasema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu.

Mtafuteni Bwana nanyi mtaishi;

Sura ya sita ya Injili ya Yohana inaanza na habari ya Yesu kulisha watu elfu tano (1-15). Baadaye kuanzia mstari wa 16, wanafunzi wanapanda chomboni kuelekea Kapernaumu. Wakiwa baharini upepo unasumbua na Yesu anawatokea akitembea juu ya maji. Kesho yake makutano walipanda mashua wakamfuata Yesu hukohuko Kapernaumu. 

Yesu akaanza kuwaambia makutano kwamba hawakumfuata kwa sababu ni Mwokozi wa ulimwengu, bali walimfuata kwa sababu walikula mikate na samaki wakashiba. Na kwa sababu hiyo akawafundisha kuwa wasikitafute chakula kiharibikacho, bali chakula kisichoharibika, yaani kumwamini Yesu mwenyewe. Ndipo Yesu akaanza kufundisha kuwa yeye ni chakula cha uzima, kilichoshuka kutoka mbinguni.

Angalia Yesu anafundisha kwamba yeye ni chakula cha uzima;

Yohana 6:48-51

48 Mimi ndimi chakula cha uzima.
49 Baba zenu waliila mana jangwani; wakafa.
50 Hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni, kwamba mtu akile wala asife.
51 Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.

Yesu anaendelea;

Yohana 6:53-56

53 Basi Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu.
54 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.
55 Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli.
56 Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake.

Somo lenyewe;

Somo linaonesha watu wengi wakipata shida na fundisho la Yesu kuwa chakula cha uzima. Yesu alifahamu, kwamba hata miongoni mwa wanafunzi wake fundisho hili lilikuwa gumu. Lakini Yesu alikuwa anajitambulisha kama Mwokozi wa ulimwengu. Yesu huyu ndiye tunayeelekezwa kumtafuta, yaani kumwamini na kumpokea mioyoni ili atuongoze, atutunze na kutupa uzima wa milele. Amina

Jumamosi njema.

Heri Buberwa