Date: 
13-08-2024
Reading: 
Amosi 9:11-15

Jumanne asubuhi tarehe 13.08.2024

Amosi 9:11-15

11 Siku hiyo nitaiinua tena maskani ya Daudi iliyoanguka, na kuziba mahali palipobomoka; nami nitayainua magofu yake, na kuyajenga kama siku za kale;

12 wapate kuyamiliki mabaki ya Edomu, na mataifa yote yaitwayo kwa jina langu, asema Bwana, afanyaye hayo.

13 Angalieni, siku zinakuja, asema Bwana, ambazo huyo alimaye atamfikilia avunaye, na yeye akanyagaye zabibu atamfikilia apandaye mbegu; nayo milima itadondoza divai tamu, na vilima vyote vitayeyuka.

14 Nami nitawarejeza tena watu wangu Israeli waliohamishwa, nao wataijenga miji iliyoachwa maganjo, na kukaa ndani yake; nao watapanda mizabibu katika mashamba, na kunywa divai yake; nao watafanyiza bustani, na kula matunda yake.

15 Nami nitawapanda katika nchi yao, wala hawatang'olewa tena watoke katika nchi yao niliyowapa, asema Bwana, Mungu wako.

Mtafuteni Bwana nanyi mtaishi;

Katika kitabu cha Amosi sura ya 9, Mungu aliwaambia Israel kwamba wangeweza kukimbia na kwenda popote lakini wasingeweza kujificha wala kuikimbia hukumu. Yaani wasingemkwepa Mungu. Ndiyo maana katika mistari kumi ya kwanza wanaambiwa kuwa mienendo yao mibaya ingesababisha waangamie. Lakini anawapa tumaini la kuwarejesha toka uhamishoni (14) maana ndiye Mungu wao.

Katika somo la leo tunaona kwamba Mungu anawakumbusha Israel kuwa ndiye Mungu wao. Anawaambia kuwa ndiye mwenye baraka, na hukumu pia. Anawaahidi kuwarejesha toka uhamishoni. Hivyo Mungu anajitambulisha kama mwanzo na mwisho kwa Israel.

Israel ya leo ni wote wamwaminio, kumpokea na kumfuata Yesu Kristo kama Bwana wao. Hatuwezi kumkwepa kwa namna yoyote, bali tumsikie na kumcha daima maana yeye ndiye mwenye hatma yetu. Amina

Jumanne njema

 

Heri Buberwa