Date: 
10-08-2024
Reading: 
Warumi 16:17-20

Jumamosi asubuhi tarehe 10.08.2024

Warumi 16:17-20

17 Ndugu zangu, nawasihi, waangalieni wale wafanyao fitina na mambo ya kukwaza kinyume cha mafundisho mliyojifunza; mkajiepushe nao.

18 Kwa sababu walio hivyo hawamtumikii Bwana wetu Kristo, bali matumbo yao wenyewe; na kwa maneno laini na ya kujipendekeza waidanganya mioyo ya watu wanyofu.

19 Maana utii wenu umewafikilia watu wote; basi nafurahi kwa ajili yenu, lakini nataka ninyi kuwa wenye hekima katika mambo mema, na wajinga katika mambo mabaya.

20 Naye Mungu wa amani atamseta Shetani chini ya miguu yenu upesi. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi. [Amina.]

Enendeni kwa hekima;

Asubuhi ya leo tunasoma juu ya kuwaepuka wale wafanyao fitina na kukwaza wengine. Paulo anasema wafanyao fitina na kuwakwaza wengine huwa hawamtumikii Bwana, bali huyatumikia matumbo yao maana husema uongo na kujipendekeza ili wafanikiwe. Paulo anasema hekima ya kweli ni kuwaepuka hao wasiomcha Bwana kwa kuachana na wajinga.

Paulo anamalizia waraka wake kwa Warumi kwa kukemea "Injili tumbo". Mambo ya uongo, fitina, chuki, usengenyaji na mambo mengine kama hayo ambayo hufanywa kwa maslahi binafsi kwa kuumiza wengine ni "Injili tumbo". Na mimi naongezea; katika kazi ya Injili, mafundisho yote ya uongo ni "Injili tumbo". Wafundishao haya hulenga kupata faida huku wakilipoteza kundi la Mungu. 

Tuwaepuke wafundisha "Injili tumbo" kama vile;

-mkomboe mzaliwa wa kwanza

-una laana za mababu

-sadaka imebeba baraka zako

-kuombea picha na nguo 

Mafundisho haya na mengine kama hayo hayana tofauti na fitina, hupoteza watu. Wanaohubiri haya hawamtumikii Bwana, bali matumbo yao.

Tuenende kwa hekima kwa kuwaepuka wote wanaoweza kutupoteza. Amina

Jumamosi njema

Heri Buberwa