Date: 
19-07-2024
Reading: 
2 Wakorintho 2:1-11

Ijumaa asubuhi 19.07.2024

2 Wakorintho 2:1-11

1 Lakini nafsini mwangu nalikusudia hivi, nisije kwenu tena kwa huzuni.

2 Maana mimi nikiwatia huzuni, basi ni nani anifurahishaye mimi ila yeye ahuzunishwaye nami?

3 Nami naliwaandikia neno lilo hilo, ili nijapo nisitiwe huzuni na wale ambao ilinipasa kuwafurahia; nikiwatumaini ninyi nyote kwamba furaha yangu ni yenu nyote pia.

4 Maana katika dhiki nyingi na taabu ya moyo niliwaandikia na machozi mengi; si kwamba mhuzunishwe, bali mpate kujua upendo wangu nilio nao kwenu jinsi ulivyo mwingi.

5 Lakini iwapo mtu amehuzunisha, hakunihuzunisha mimi tu, bali kwa sehemu (nisije nikalemea mno), amewahuzunisha ninyi nyote.

6 Yamtosha mtu wa namna hii adhabu ile aliyopewa na walio wengi;

7 hata kinyume cha hayo, ni afadhali mmsamehe na kumfariji, mtu kama huyo asije akamezwa katika huzuni yake ipitayo kiasi.

8 Kwa hiyo nawasihi kumthibitishia upendo wenu.

9 Maana naliandika kwa sababu hii pia, ili nipate bayana kwenu kwamba mmekuwa wenye kutii katika mambo yote.

10 Lakini kama mkimsamehe mtu neno lo lote, nami nimemsamehe; kwa maana mimi nami, ikiwa nimemsamehe mtu neno lo lote, nimemsamehe kwa ajili yenu mbele za Kristo,

11 Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake.

Wito wa kuwajali wengine katika Kristo;

Mtume Paulo anawaandikia Wakorintho kuishi katika furaha ya Kristo. Anawataka kutoishi katika huzuni, na hata ikitokea mtu akawasababishia huzuni wamsamehe. Anawasihi kuthibitisha upendo wao kwa wote, wakiwemo wasababishao huzuni. Kwa ujumla wake, Mtume Paulo anasisitiza watu wa Korintho kuwa na msamaha.

Ujumbe tunaopewa asubuhi ya leo ni kukaa pamoja tukisaidiana, tukivumiliana na kusameheana. Msamaha tunaoambiwa ni kusamehe watu wote wanaotukosea. Tunawajibika kusamehe kama Yesu alivyosema;

Marko 11:25-26

25 Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu.
26 Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.]

Tuwajali wengine kwa upendo na msamaha katika Kristo Yesu. Amina.

Ijumaa njema

 

Heri Buberwa