Alhamisi asubuhi tarehe 27.06.2024
Mwanzo 50:15-21
15 Ndugu zake Yusufu walipoona ya kwamba baba yao amekufa, walisema, Labda Yusufu atatuchukia; naye atatulipa maovu yetu tuliyomtenda.
16 Wakapeleka watu kwa Yusufu, kunena, Baba yako alitoa amri kabla ya kufa kwake, akasema,
17 Mwambieni Yusufu hivi, Naomba uwaachilie ndugu zako kosa lao na dhambi yao, maana walikutenda mabaya; sasa twakuomba utuachilie kosa la watumwa wa Mungu wa baba yako. Yusufu akalia waliposema naye.
18 Nduguze wakaenda tena, wakamwangukia miguu, wakasema, Tazama, sisi tu watumwa wako.
19 Yusufu akawaambia, Msiogope, je! Mimi ni badala ya Mungu?
20 Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo.
21 Basi sasa msiogope; mimi nitawalisha na watoto wenu. Akawafariji, na kusema nao vema.
Iweni na huruma;
Wana wa Yakobo walikuwa na hofu kwamba baada ya baba yao kufa wangetendwa ubaya na Yusufu (kumbuka walimuuza Yusufu kwa Wamisri). Walituma watu kuongea na Yusufu, wakaenda pia kumwangukia ili asije kulipiza kisasi dhidi yao. Hii yote ilikuwa ni kujiokoa na walichokiona kisasi cha Yusufu kikija mbele yao.
Lakini Yusufu mwenyewe wala hakuwa na mawazo hayo. Anasema yeye siyo badala ya Mungu (19). Katika mstari wa 21 anaahidi kuwatunza na kuwalisha wao na jamaa yao yote. Yusufu hapa alionesha huruma kama Bwana alivyomuongoza, akawa faraja kwa ndugu zake. Usilipize kisasi, kuwa na huruma. Amina
Alhamisi njema
Heri Buberwa