Jumatano asubuhi tarehe 19.06.2024
Yohana 17:20-21
20 Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao.
21 Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma.
Umoja wetu, nguvu yetu;
Ni dhahiri kuwa watu wanapokuwa pamoja hufanikiwa sana kuliko mtu akifanya jambo peke yake, hasa katika taasisi au kundi lenye uhitaji wa kufikia lengo ambalo faida yake ni kwa wote. Mtume Paulo aliandika;
Waefeso 4:5-7
[5]Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. [6]Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote. [7]Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo.Mtume Paulo anawaambia waefeso kuwa ni Bwana mmoja, Imani moja, na ubatizo mmoja. Mtume Paulo anamaanisha kuwa Mungu nwenyewe ametufanya kuwa wamoja. Anatuhimiza kila mmoja kutumia kipawa chake kudumisha umoja.
Sura ya 17 ya Injili ya Yohana ni sala, ambayo ni hitimisho la mafundisho yake katika sura ya 14 hadi 16. Ni baada ya sala hii Bwana Yesu alikamatwa na kusulibiwa. Ni maoni yangu kuwa, sala hii ambayo ni sala ndefu ya Bwana Yesu iliyoandikwa miongoni mwa sala alizosali, ililengwa kusikika na wanafunzi wake, moja ya lengo likiwa ni kuleta faraja na tumaini, kwa mioyo ya wanafunzi iliyovunjika, ya wanafunzi. Somo la leo linaonyesha kuwa sala hii haikuwa kwa ajili ya wanafunzi tu, bali kwa wakristo wa vizazi vyote.
Yohana 17:20-21
[20]Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao. [21]Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma.Hivyo, Yesu alituombea sisi sote.
Tunapoiangalia sala hii, kinachonijia ni mstari wa kwanza wa sura hii ya 17;
Yohana 17:1
[1]Maneno hayo aliyasema Yesu; akainua macho yake kuelekea mbinguni, akasema, Baba, saa imekwisha kufika. Mtukuze Mwanao, ili Mwana wako naye akutukuze wewe;
Ili kuona kwa nini nafikiria mwanzo wa sala hii ni muhimu kwa Kanisa, jiulize; Baba atamtukuzaje Mwana, ili naye amtukuze yeye?
Kumbuka Yesu anasema "saa imekwisha". Ni saa ipi? Ni saa ya kifo chake. Hivyo Yesu anapoongelea kutukuzwa, na kumtukuza Baba yake, msingi wa mwanzo ni Yesu kufa msalabani. Utukufu wa Mwana unaonekana, na wa Baba vivyo hivyo, Yesu anapokufa msalabani kama Sadaka, kama mchambuzi mmoja alivyowahi kuandika;
"Msalaba ni Utukufu wa Mungu, kwa sababu Yesu kujitoa sadaka ni upendo kamili" (William Temple 2:308)
Yesu alimtukuza Mungu kupitia mateso na kifo. Kanisa linaelekezwa kumtukuza Mungu. Mtume Paulo anaandika;
1 Wakorintho 10:31
[31]Basi, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.Kanisa lazima likumbuke kuwa linaitwa kujitoa katika hali yoyote, katika wakati wowote, kwa Mungu. Utukufu tunaompa Mungu kama waaminio na Kanisa kwa ujumla, ni kupitia sadaka, na sio kupitia ukuu wetu hapa duniani. Sadaka inayoongelewa hapa ni zaidi ya matoleo. Ni kujitoa kwa Mungu ipasavyo. Ni kupitia ugonjwa, maumivu, sadaka, na mengine kama hayo, Utukufu wa Mungu unaonekana, maana sio kwamba Mungu anatukuzwa tukiumia, bali Utukufu wa Mungu unaonekana kupitia maumivu, sadaka, udhaifu n.k
Yesu na mitume hawakumpa Mungu Utukufu katika Palestina kwa kuvaa vizuri, kwa nyumba kubwa na nzuri, au kwa mali nyingi, labda na mahekalu ya gharama. Utukufu wa Mungu ulionekana kupitia kwa Yesu, ambaye hakuwa na sehemu ya kulaza kichwa chake, aliposulibiwa.
"....Imani yetu ni kama kundi la nyota nyota angani. Kundi la nyota likionekana dogo, linakuwa juu sana. Vivyo hivyo, kwa mkristo aishiye katika dunia hii, ili awe mkubwa katika dunia hii, lazima aonekane mdogo na dhaifu, akiwa mnyenyekevu" (Soren Kierkegaard in Practice in Christianity; pg 198)
Lazima tufahamu kuwa njia ya kumtukuza siyo nyepesi. Ina mabonde mengi na milima. Tunapoiendea njia ya kumtukuza Mungu wetu, tuuweke ukuu wa dunia pembeni.
Nimetumia muda kuelezea kumpa Mungu utukufu, maana ni njia ya kumwendea Mungu, ambapo Yesu analikumbusha Kanisa kumuendea yeye, na hatimaye Kanisa lake liwe na umoja, kama alivyotuombea.
Yesu aliliombea umoja Kanisa lake (somo la leo). Kama kuna mtu labda anafikiria Yesu asingefanya hili, atakuwa hajafuatilia historia ya Kanisa. Yesu alichokitaka, ambacho kimekuwa kigumu kwa Kanisa, ni Kanisa kuwa na Umoja, kama mfano wa Mungu mwenyewe. Kanisa linapashwa kuwa na umoja, kama Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, yaani muungano wa upendo, ushirika, na malengo ya pamoja.
Kwa msomaji wa Agano jipya, utakuwa umekutana na mambo yahusuyo umoja, kama vile kutofautiana kimtazamo kwenye mafundisho (Theologia), watu kugombana, tofauti za makundi, viongozi kutumia madaraka vibaya na kuharibu Kanisa, waumini kulalamika na kufanya mambo yaliyoligawa Kanisa n.k Pamoja na Agano jipya kulinda ujumbe wa Yesu usipotoshwe, Agano jipya linaelekeza wakristo kuungana pamoja, na yeyote anayesababisha kutokuwa na umoja hafai, kama Mtume Paulo anavyomwandikia Tito;
Tito 1:16
[16]Wanakiri ya kwamba wanamjua Mungu, bali kwa matendo yao wanamkana; ni wenye machukizo, waasi, wala kwa kila tendo jema hawafai.Mungu anatuita kuwa pamoja katika utume huu. Ni wakati wa kumaliza tofauti zetu. Twaweza kutofautiana na mambo mbalimbali lakini tukaendelea kuheshimiana na kupendana.
Tunaitwa kumwendea Mungu, ili tujawe na hofu ya Mungu itakayosababisha tupendane, tuwe na umoja.
Katika sala hii, Yesu anatufundisha nini?
1. Yesu alikuwa na uhusiano mzuri na Baba yake;
Hii inaonekana kwa sababu Yesu anamuomba Baba yake. Kanisa linaitwa kuwa na uhusiano mzuri na Mungu, maana Kanisa ni la Mungu mwenyewe. Kanisa kama kundi la waaminio, ni watu ambao lazima wawe na umoja, ili kutekeleza ombi la Bwana Yesu, ambapo Kanisa likishakuwa na umoja, litakuwa moja tu, hivyo uhusiano wetu na Mungu kuwa mzuri kwa kuwa tutakuwa wamoja kama Mungu wetu anavyotaka.
2. Yesu aliishi maisha halisi.
Pamoja na kwamba Bwana Yesu alikuwa Mungu kweli, aliomba. Alitufundisha kuomba. Alichangamana na watu wote, hadi kuna wakati aliulizwa ni kwa nini anakaa na wenye dhambi?
Sisi tunaishi maisha halisi ya Yesu?
Tunapendana?
Maisha yetu yanaakisi umoja aliotuombea Yesu?
3. Yesu alikuwa mnyenyekevu.
Yohana 17:4
[4]Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye.Sisi tunamtumikia Mungu kwa unyenyekevu? Au tunaishia kujikweza tu? Tunamtukuza Mungu kwa kazi zetu? Kijishusha kunatufanya tuonekane sawa, hivyo kuwa wamoja.
4. Yesu alikuwa na upendo wa ajabu.
Yohana 17:26
[26]Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao.Pendo la Yesu likiwa ndani yetu tunakuwa wamoja. Upendo wa Kristo lazima uonekane miongoni mwetu, kama Kanisa la Kristo. Mfano halisi wa upendo ni Yesu mwenyewe Yesu mwenyewe aliyejitoa sadaka kwa ajili ya Kanisa lake. Nasi tuuige mfano huu wa Yesu, yaani upendo udumu kati yetu.
Hapa ni kila mmoja wetu kujihoji, kama anao upendo wa Yesu Kristo.
5. Yesu alikuwa na ushuhuda wa kweli;
Yohana 17:17
[17]Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.Maisha yetu lazima yashuhudie ukweli wa neno la Mungu. Umoja tunaoitwa kuwa nao, ni katika Kristo. Hatuwezi kuwa na huo umoja wa Kristo, pasipo neno la Kristo mwenyewe kushuhudiwa kupitia maisha yetu.
6. Bwana Yesu alituombea umoja
Yohana 17:20-23
[20]Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao. [21]Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. [22]Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. [23]Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi.Hapa ndipo ulipo mkazo wa somo la siku ya leo;
Tukae pamoja kwa umoja.
Bwana Yesu aliomba tuwe na umoja. Kwetu sisi hili ni agizo. Kanisa la Mungu linakumbushwa kuwa na umoja. Kanisa ni sisi waaminio, mmoja mmoja, hadi kundi kubwa. Tunaitwa kuishi pamoja kwa upendo, ili tuweze kuwa pamoja katika kuitenda kazi ya Mungu. Yesu anatuagiza kuwa na umoja ili kuleta utengemano kwenye Taifa la Mungu, yaani watu. Ni juu yetu kutafakari kama tunao umoja huu anaotuagiza Yesu kuwa nao. Kifungo chetu kiwe upendo, tukitumia vipawa yeti kuifanya kazi ya Mungu, tukiutunza umoja wetu.
Tunaudumishaje umoja huu?
i) Tusimame katika neno la Mungu, maana msingi wa Kanisa ni neno la Mungu, yaani Biblia isiyo na mbadala. Tusimame imara kuanzia kwenye familia zetu, tukisoma na kujifunza neno la Mungu, ili umoja wetu udumu katika neno la Kristo.
ii) Tujitoe kwa ajili ya kazi ya Mungu.
Tunawajibika kujitoa sisi na kumtolea Mungu mali alizotupa kwa ajili ya kazi yake. Kanisa lina wajibu mkubwa wa kuihudumia jamii katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, afya, mazingira, maji, wasiojiweza, uchumi n.k Huduma zote hizi na nyinginezo zinahitaji fedha. Kazi za umoja zinaliunganisha Kanisa katika kutekeleza huduma ya diakonia. Sasa, ili kazi hizi ziweze kuendelea kwa ufanisi, tumtolee Mungu aliyetupa, ili Injili iwafikie wengi, kundi la Bwana lizidi kukua, ili kuitimiza sala ya Yesu, yaani " wote wakujue wewe" Kazi kubwa ya Kanisa ni kuhubiri Injili. Tukiungana, tunakuwa na nguvu kubwa ya kuhubiri. Hivyo kwa umoja wetu, tukae pamoja, tumtangaze Kristo kadri tunavyoweza.
iii) Tutunze taratibu zetu.
Hakuna sehemu isiyokuwa na utaratibu.
Hata wezi na majambazi wana utaratibu wao, yaani tusipokuwa na utaratibu tunazidiwa na majambazi. Wanapanga, wanaenda kwa pamoja!
Utunzaji wa umoja wetu ni kupitia kutunza taratibu ambazo zimewekwa ili umoja wetu usitereke.
Katekismo ifundishwe kwa ukamilifu wake ili watu wajue msingi wa Imani yetu, na siyo kulipua mafundisho, hatimaye waumini wanatangatanga. Hakuna mtu aliyefundishwa vizuri Katekismo, na matengenezo ya Kanisa anaweza kutangatanga ovyo.
Utaratibu wa ibada uheshimiwe;
Mojawapo ya makubaliano ya wazee waliounda KKKT ilikuwa ni kuwa na ibada za aina moja. Hili linatunzwa? Tuna ibada za aina moja?
Imefikia hatua Mchg au Mwinjilisti akitoka usharikani au mtaani kwake hawezi kwenda pengine akaongoza ibada peke yake, lazima awe na mwenyeji, maana utaratibu wa ibada haujulikani.
Hapa nasimama, Mungu nisaidie;
Siku hizi kuna ibada za ajabu ajabu! Mambo ya "kipuuzi" yameingizwa Kanisani. Hoja ikiwa eti Roho Mtakatifu ndiye anayemuongoza mtumishi ibada iendeje. Eti tusimpangie Roho Mtakatifu! Una uhakika utaratibu huo umeanza leo? Ni mpya? Ina maana Roho Mtakatifu akikuongoza ndipo unasali kwa kelele? Roho Mtakatifu anataka tusali kwa kelele? Yaani sisi leo tuna Roho Mtakatifu kuliko wale wazee walioongozwa na Askofu Moshi? Mbona maono yao ndio yanaishi hadi leo? Sisi tumefanya nini jipya?
Hizo hoja mufilisi zinajengwa na kikundi cha watu waliojichomeka Kanisani kufanya ujasiliamali! Wakifanya maigizo yao pale mbele, wakanena kwa lugha zisizojulikana na kuombea nguo (upuuzi) wanalipwa chao, yaani wana malengo binafsi. Shida inakuja kwenye tafsiri na mafundisho, hasa ya Agano jipya. Wanaombea nguo, ila ng'e na nyoka hawakanyagi, chakula cha sumu hawali, matapeli!
Taratibu za ibada ziheshimiwe, zitunzwe ili kutunza umoja wetu, maana taratibu hizo hazikuwahi kuharibu ushuhuda wa Kanisa. Ushuhuda wa Kanisa ukipotea, maana yake hata ushuhuda wa Mkristo mmoja mmoja utapotea, hivyo umoja wetu kuwa shakani.
Namaliza kwa kusema kuwa;
-Umoja wa Kikristo sio taasisi tu, bali ni maisha ya pamoja ndani ya Yesu Kristo.
-Umoja wa Kikristo ni muhimu, maana ni sababu ya ushuhuda wetu, ili wengi wamuamini Yesu Kristo.
-Umoja wa Kikristo unaonekana kwa waaminio, wenye upendo, malengo ya pamoja na ujumbe wa wokovu katika Yesu Kristo.
Tunaitwa kutunza umoja aliotuachia Yesu.
Nini nafasi yako katika kutunza umoja wa Kanisa?
Bwana akubariki.
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650