Date: 
04-06-2024
Reading: 
Yeremia 10:1-10

Jumanne asubuhi tarehe 04.06.2024

Yeremia 10:1-10

1 Enyi nyumba ya Israeli, lisikieni neno awaambialo Bwana;

2 Bwana asema hivi, Msijifunze njia ya mataifa, wala msishangae kwa sababu ya ishara za mbinguni; maana mataifa hushangaa kwa sababu ya ishara hizo.

3 Maana desturi za watu hao ni ubatili, maana mtu mmoja hukata mti mwituni, kazi ya mikono ya fundi na shoka.

4 Huupamba kwa fedha na dhahabu; huukaza kwa misumari na nyundo, usitikisike.

5 Mfano wao ni mfano wa mtende, kazi ya cherehani, hawasemi; hawana budi kuchukuliwa, kwa sababu hawawezi kwenda. Usiwaogope; kwa maana hawawezi kutenda uovu, wala hawana uwezo wa kutenda mema.

6 Hapana hata mmoja aliye kama wewe, Ee Bwana; wewe ndiwe uliye mkuu, na jina lako ni kuu katika uweza.

7 Ni nani asiyekucha wewe, Ee mfalme wa mataifa? Maana hii ni sifa yako wewe; kwa kuwa miongoni mwa wenye hekima wote wa mataifa, na katika hali yao ya enzi yote pia, hapana hata mmoja kama wewe.

8 Lakini wote pia huwa kama wanyama, ni wapumbavu. Haya ni maelezo ya sanamu, ni shina la mti tu.

9 Iko fedha iliyofuliwa ikawa mabamba, iliyoletwa kutoka Tarshishi, na dhahabu kutoka Ufazi, kazi ya stadi na ya mikono ya mfua dhahabu; mavazi yao ni rangi ya samawi na urujuani; hayo yote ni kazi ya mafundi yao.

10 Bali Bwana ndiye Mungu wa kweli; Ndiye Mungu aliye hai, Mfalme wa milele; Mbele za ghadhabu yake nchi yatetemeka, Wala mataifa hawawezi kustahimili hasira yake.

Chagueni mtakayemtumikia;

Asubuhi hii tunamsoma Yeremia akileta ujumbe kwa Taifa la Mungu unaowataka watu kutojifunza njia ya mataifa. Anawataka kutoshangaa kwa sababu ya ishara za mbinguni, maana mataifa hushangaa kwa sababu ya ishara hizo. Yeremia anawaambia watu kuwa hakuna aliye kama Bwana aliye Mkuu na muweza, na kwa sababu hiyo anawaita kumcha Bwana.

Yeremia anahitimisha kwa kusema kuwa Bwana ndiye Mungu wa kweli, Mungu aliye hai, Mfalme wa milele. Ni wito kwetu leo kumcha Bwana aliye Mfalme wa milele. Tunamcha Bwana tunapochagua kuishi kwa kumwamini yeye. Tuchague kumtumikia Bwana aliye Mungu wa kweli, sasa na siku zote. Amina

Jumanne njema 

 

Heri Buberwa 

Mlutheri