Jumamosi asubuhi tarehe 25.05.2024
2 Wakorintho 6:14-17
14 Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?
15 Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini?
16 Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
17 Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha.
Roho Mtakatifu kwa kila aaminiye;
Mtume Paulo anawaandikia Wakorintho kuwa wasifungiwe nira na wasioamini, kwa maana hapana urafiki kati ya haki na uasi. Paulo anakazia kuwa hakuna mapatano kati ya hekalu la Mungu na sanamu maana wao waaminio ni hekalu la Mungu aliye hai. Kwa hiyo anawaita waaminio kutoka kati ya wasioamini maana ni sawa na kugusa kitu kilicho kichafu.
Neno tulilosoma linatumika sana na baadhi ya waamini hasa wajionao wameokoka kuliko wengine. Hujiona wana Roho Mtakatifu, hivyo kujitenga na wengine. Inafikia hata salamu inatolewa kwa kuchagua, anayeonekana kuokoka anasalimiwa "Bwana Asifiwe", asiyeokoka anasalimiwa "habari za saa hizi"! Hiyo siyo maana yake! Naamini sisi sote ni wenye dhambi, ambao tumeokolewa kwa neema. Ujumbe muhimu kwa somo hili siyo kujitenga, bali ni "kuichukia dhambi, na kumpenda mwenye dhambi, maana sisi sote tu wenye dhambi". Amina
Jumamosi njema
Heri Buberwa