Date: 
14-05-2024
Reading: 
Luka 18:1-6

Jumanne asubuhi tarehe 14.05.2024

Luka 18:1-6

1 Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa.

2 Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu.

3 Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu.

4 Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu,

5 lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima.

6 Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu.

Omba! Mungu anasikia kuomba kwetu!

Yesu anatoa mfano wa mwanamke mjane aliyemwendea kiongozi kuomba haki yake aliyokuwa akistahili toka kwa adui yake. Yule kiongozi alikataa, lakini yule mjane hakuacha kutokea mbele yake. Aliamua kumpa haki yake mjane ili asiendelee kumuudhi. 

Yesu anasema kama kiongozi tu anampa haki aombaye bila kuchoka, iweje tukiomba kwa Mungu? Yesu anasema;

Luka 18:7-8

7 Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?
8 Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?

Ujumbe wa Yesu kama anavyoanza katika mstari wa kwanza ni kumuomba Mungu bila kukata tamaa. Asubuhi hii Yesu anatupa uhakika wa kusikia maombi yetu, lakini anatukumbusha kumuomba kwa imani. Kwa hiyo Omba! Mungu anasikia kuomba kwako. Amina.

Jumanne njema 

 

Heri Buberwa