Date:
09-05-2024
Reading:
Marko 16:19-20
Alhamisi tarehe 09.05.2024
Siku ya kukumbuka kupaa kwa Bwana Yesu Kristo;
Masomo;
Zab 68:17-20
Efe 1:15-23
*Mk 16:19-20
Marko 16:19-20
19 Basi Bwana Yesu, baada ya kusema nao, akachukuliwa juu mbinguni, akaketi mkono wa kuume wa Mungu.
20 Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.]
Kristo amepaa katika Utukufu wake;
Somo la leo ni hitimisho la Injili ya Marko. Kwa ufupi wake, ni jinsi Yesu alivyomaliza kazi yake hapa duniani. Somo linatueleza Yesu alikokwenda, lini aliondoka na alivyopaa kurudi mbinguni. Somo pia linatuonyesha kazi waliyofanya wanafunzi baada ya kiongozi wao kuwaacha.
Yesu alikwenda wapi?
Kama tulivyosoma, alichukuliwa mbinguni akaketi mkono wa kuume wa Mungu. Alirudi katika Utukufu aliokuwa nao kabla hajaja duniani kama Mpatanishi na Mwokozi. Huko hukaa hata leo, akiendelea kuwapokea wote wamjiao na kuwaokoa;
Waebrania 7:25
[25]Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee.Hadi hapo ipo faraja kwa waaminio, ambao huishi katika dunia hii. Tabu na shida ziko nyingi sana, na kushindwa pia. Lakini faraja ya kweli ipo, ambaye ni Yesu Kristo anayeishi hadi sasa. Hivyo kupaa kwa Yesu siyo kwamba alituacha, bali hutenda kazi milele yote.
Tunapashwa kufahamu kuwa kupaa kwa Yesu kuliashiria kumalizika kwa kazi ya Yesu hapa duniani, kama Mwanadamu kweli na Mungu kweli. Alifanya kazi ya kuleta wokovu kwa ukamilifu. Yaani hadi Yesu anapaa, aliacha ujumbe wa wokovu unaojitosheleza. Hapa ndipo Yesu anatutuma kuitenda kazi yake, ili kuuendeleza utume wa kuwaokoa watu wake. Tunatimiza wajibu huu?
Kama tulivyosoma, wanafunzi wake walilitimiza hilo. Walitoka na kuhubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao. Nini nafasi yetu katika hili? Sisi kama Kanisa la Mungu tunaifanya kazi hii ya utume kwa ukamilifu? Hapa nataka kuonesha kuwa kupaa kwa Yesu ilikuwa ishara ya kututuma sisi kuuendea utume.
Katika huduma yetu ni muhimu kuzingatia;
-Yatupasa tuwe na baraka zake katika maisha na huduma yetu kwa ujumla kama Yesu alivyotubariki.
-Tumwabudu kabla na baada ya kazi zake. Yaani tumwabudu wakati wote.
Wanafunzi walienda zaidi ya siku 40 za kuwa pamoja na Kristo mfufuka wakitafakari katika kupaa kwa mtazamo mpya kwa Utukufu wa Mungu. Waumini wote wa kweli wana uelewa wa kuuona Utukufu wa Mungu katika Kristo Yesu. Tunapouona Utukufu wa Mungu kwa Yesu aliyefufuka na kupaa, tujazwe ibada, furaha na shukrani kwa Mungu kwa ajili ya rehema. Kama bado unakosa vitu hivi, omba Yesu atimize haja ya moyo wako. Mtafute yeye bila kuchoka.
Mwisho;
Kama tukirivyo katika ukiri wa Imani;
"...Siku ya tatu akafufuka kutoka kwa wafu, akapaa mbinguni, ameketi mkono wa kuume wa Mungu Baba Mwenyezi, kutoka huko atakuja kuwahukumu walio hai na wafu..." Tuadhimishe na kukumbuka kupaa kwa Yesu tukijua kuwa Yesu atarudi tena. Hivyo unawajibika kujiandaa ili Yesu akirudi usiachwe.
Heri Buberwa Nteboya
Ascension 2024