Date: 
07-05-2024
Reading: 
2 Mambo ya nyakati 7:11-14

Jumanne asubuhi tarehe 07.05.2024

2 Mambo ya Nyakati 7:11-14

11 Hivyo Sulemani akaimaliza nyumba ya Bwana, na nyumba ya mfalme; na yote yaliyomwingia Sulemani moyoni ayafanye nyumbani mwa Bwana, na nyumbani mwake mwenyewe, akayafanikisha.

12 Bwana akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu.

13 Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni;

14 ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.

Ombeni nanyi mtapata;

Suleimani baada ya kufanya sala, utukufu wa Bwana ulishuka ukalijaza hekalu. Suleimani akawaongoza watu kutoa sadaka mbele za Mungu. Katika somo tunaona Mungu akimwambia Suleimani kuwa ameisikia sala yake. Mungu anaahidi kupitia kwa Suleimani kusikia sala za watu wake watakapomuomba kwa unyenyekevu na kuacha uovu.

Mungu aliwaahidi wana wa Israeli kusikia sala yao, pale wangemcha na kuacha uovu. Mpango wa wokovu uliendelea, ambapo baada Yesu kuja alifundisha kuomba kwa jina lake;

Yohana 14:13-14

13 Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.
14 Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.

Ukiangalia jumlisho la somo tulilosoma toka Mambo ya Nyakati ni kuacha uovu na kuwa wanyenyekevu ili kumuomba Mungu. Kuacha uovu kunakotajwa hapa ni kuwa na imani ya kweli katika Kristo. Hivyo tunaelekezwa kuomba kwa imani, kwa jina la Yesu Kristo. Amina.

Jumanne njema 

 

Heri Buberwa 

Mlutheri