Date: 
29-04-2024
Reading: 
Sefania 3:14-15

Jumatatu asubuhi tarehe 29.04.2024

Sefania 3:14-15

14 Imba, Ee binti Sayuni; piga kelele, Ee Israeli; Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, Ee binti Yerusalemu.

15 Bwana ameziondoa hukumu zako, Amemtupa nje adui yako; Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati yako; Hutaogopa uovu tena.

Njooni tumwimbie Bwana;

Baada ya manabii Isaya na Mika, ilipita miaka kama sabini bila Yuda kuwa na Nabii hadi alipotokea Sefania. Katika kipindi hicho Mfalme Manase alitawala kwa muda wa miaka 55. Utawala wake ulirudisha Yuda nyuma kiroho. Desturi za dini ya miungu, ukatili na mauaji vilienea katika utawala wake (2Fal 21,23)

Mwanawe Amoni alipotawala alifuata mwongozo mbaya wa baba yake. Aliuawa baada ya kutawala miaka miwili (2Fal 21:19-26). Yosia mwanawe akawekwa katika utawala akiwa na umri wa miaka minane (2Fal 22:1-2). Yosia akiwa bado mdogo, Sefania alianza kutoa unabii. Mfalme Yosia alipofikisha umri wa miaka 20 akafanya Matengenezo kidini na kisiasa.

Ujumbe wa Sefania ni "Siku ya Bwana" ambayo itatakasa uovu wote katika mataifa yote. Uovu wa Yuda ni kuabudu miungu na kukosa uadilifu. Yuda inatolewa wito wa kutubu (2:3). Hukumu kwa mataifa ni fundisho kwa Yuda (sura ya 3). Sefania anaahidi wokovu kwa "mabaki" ya Yuda hasa watiifu na wanyenyekevu. "Mabaki" yatafurahia baraka za Bwana.

Sehemu tuliyosoma, ni ahadi ya Bwana kuwasamehe watu wake, na kuwaahidi maisha mapya ya wokovu. Ni katika maisha hayo watu wanapewa Ujumbe wa kumsifu Bwana. Tunaalikwa kumsifu Bwana daima, yaani maisha yetu kuwa yenye Utukufu kwa Bwana. Amina.

Tunakutakia wiki njema 

 

Heri Buberwa