Date: 
25-04-2024
Reading: 
Zaburi 91:1-10

Alhamisi asubuhi tarehe 25.04.2024

Zaburi 91:1-10

1 Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi.

2 Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini.

3 Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo.

4 Kwa manyoya yake atakufunika, Chini ya mbawa zake utapata kimbilio; Uaminifu wake ni ngao na kigao.

5 Hutaogopa hofu ya usiku, Wala mshale urukao mchana,

6 Wala tauni ipitayo gizani, Wala uele uharibuo adhuhuri,

7 Ijapo watu elfu waanguka ubavuni pako. Naam, kumi elfu mkono wako wa kuume! Hata hivyo hautakukaribia wewe.

8 Ila kwa macho yako utatazama, Na kuyaona malipo ya wasio haki.

9 Kwa kuwa Wewe Bwana ndiwe kimbilio langu; Umemfanya Aliye juu kuwa makao yako.

10 Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako.

Maisha mapya ndani ya Kristo;

Zaburi hii ni tumaini kwa amtumainiye Mungu kushinda majaribu. Iko wazi kwenye mstari wa kwanza na wa pili, kwamba akaaye chini ya uvuli wa Mwenyezi Mungu atashinda. Inaendelea kuonekana kuwa Bwana atakuwa kimbilio la yule amtumainiye. Hofu wala tauni havina nafasi kwao wamtumainio Bwana, maana yeye (Bwana) ndiye kimbilio lao. 

Ukisoma zaidi unaona maneno aliyotumia shetani kumjaribu Yesu;

Zaburi 91:11-13

11 Kwa kuwa atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote.
12 Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.
13 Utawakanyaga simba na nyoka, Mwana-simba na joka utawaseta kwa miguu.

Waweza kukumbuka hapa;

Mathayo 4:6-7

6 akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.
7 Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako.

Hapa Yesu alishinda majaribu kwa neno la Mungu.

Tunashinda majaribu kwa kumkimbilia na kumtumaini Bwana, kwa njia ya neno lake. Tukilishika neno lake maisha yetu yanakuwa mapya wakati wote. Amina

Alhamisi njema.

Heri Buberwa