Date: 
23-04-2024
Reading: 
Isaya 11:1-9

Jumanne asubuhi tarehe 23.04.2024

Isaya 11:1-9

1 Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda.

2 Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana;

3 na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake;

4 bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya.

5 Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia.

6 Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza.

7 Ng'ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng'ombe.

8 Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira.

9 Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari.

Maisha mapya ndani ya Kristo;

Ni mwendelezo wa Isaya akitabiri ujio wa Yesu Kristo ulimwenguni. Anamtabiri Yesu kama Mfalme, Mwokozi na mtawala kwa watu wote. Kristo huyu anatajwa kuwa mwenye hukumu za haki, aonyaye kwa upendo na kwa adili. Wote wamwaminio wanatajwa kuishi kwa tumaini na upendo katika umoja wa Kikristo.

Yesu huyu aliyetabiriwa na Nabii Isaya ndiye katika majira haya tunaadhimisha kufufuka kwake. Aliitimiza kazi ya kuukomboa ulimwengu kama ilivyotabiriwa na Nabii Isaya. Tunasoma katika Matendo ya Mitume jinsi inavyodhihirika;

Matendo ya Mitume 13:23

Katika uzao wake mtu huyo Mungu amewaletea Israeli Mwokozi, yaani, Yesu, kama alivyoahidi;

Tumwamini Yesu mfufuka ili tuwe na maisha mapya katika yeye. Amina.

Jumanne njema.

Heri Buberwa