Date: 
19-04-2024
Reading: 
Isaya 43:1-7

Ijumaa asubuhi tarehe 19.04.2024

Isaya 43:1-7

1 Lakini sasa, Bwana aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu.

2 Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza.

3 Maana mimi ni Bwana, Mungu wako; Mtakatifu wa Israeli, mwokozi wako, nimetoa Misri kuwa ukombozi wako; nimetoa Kushi na Seba kwa ajili yako.

4 Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na kabila za watu kwa ajili ya maisha yako.

5 Usiogope; maana mimi ni pamoja nawe; nitaleta wazao wako toka mashariki, nitakukusanya toka magharibi;

6 nitaiambia kaskazi, Toa; nayo kusi, Usizuie; waleteni wana wangu kutoka mbali, na binti zangu kutoka miisho ya dunia.

7 Kila mmoja aliyeitwa kwa jina langu, niliyemwumba kwa ajili ya utukufu wangu; mimi nimemwumba, naam, mimi nimemfanya.

Bwana huchunga na kulisha kundi lake;

Bwana kupitia Nabii Isaya anawaambia Israeli wasiogope, maana yeye ndiye aliyewakomboa. Yeye ndiye Bwana wao. Ujumbe huu ulitolewa wakati Israeli wakiwa uhamishoni, ndiyo maana ni ujumbe wa faraja. Israeli wanapewa uhakika wa kuepushwa na hatari zote. Bwana anawatoa wasiwasi akiwakumbusha jinsi alivyowatoa utumwani Misri. 

Ukiendelea kusoma unazidi kuiona ahadi ya ukombozi;

Isaya 43:13-14

13 Naam, tangu siku ya leo, mimi ndiye; wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu; mimi nitatenda kazi, naye ni nani awezaye kuizuia?
14 Bwana, Mkombozi wenu, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Kwa ajili yenu nimetuma ujumbe Babeli nami nitawashusha wote mfano wa wakimbizi, naam, Wakaldayo, katika merikebu zao walizozifurahia.

Somo letu tunaona kwamba ulikuwa ni ujumbe wa faraja kwa Israeli wakati ule wako uhamishoni. Ujumbe mkuu ulikuwa ni Bwana kutowaacha (Israeli).

Ujumbe huu unadumu hata sasa, ambapo Yesu aliye Mwokozi wetu hukaa nasi siku zote tukimpokea na kumwamini. Yeye hutuchunga na kutulisha malishoni mwake, yaani kuwa nasi daima katika njia ya ufuasi kuelekea uzima wa milele. Amina

Ijumaa njema 

Heri Buberwa