Date: 
17-04-2024
Reading: 
1Petro 5:1-4

Jumatano asubuhi tarehe 17.04.2024

1 Petro 5:1-4

1 Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye;

2 lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo.

3 Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi.

4 Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka.

Bwana huchunga na kulisha kundi lake;

Petro anamalizia waraka wake wa kwanza akiwataka viongozi wa Kanisa kulichunga Kanisa la Mungu kama walivyopewa utume huo na Kristo mwenyewe. Anawataka kuchunga kundi la Mungu kwa hiari yao kama Mungu atakavyo, si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo.

Petro anakemea kujifanya bwana juu ya wanaoongozwa, ili Kristo aliye Mchungaji mkuu akidhihirishwa tuipokee taji ya utukufu. 

Wito wa Petro ni kuitenda kazi ya Mungu kwa uaminifu, kila mtu kwa nafasi yake. Kristo aliye Mchungaji mkuu anatuita kuwa mashahidi wema katika kujenga Kanisa lake, ili Ufalme wake uenee pote. Kuwa shahidi wa Kristo ili kuujenga Ufalme wake. Amina.

Jumatano njema.

Heri Buberwa