Date: 
13-04-2024
Reading: 
Mwanzo 7:1-5

Jumamosi asubuhi tarehe 13.04.2024

Mwanzo 7:1-5

1 Bwana akamwambia Nuhu, Ingia wewe na jamaa yako yote katika safina; kwa maana nimekuona wewe u mwenye haki mbele zangu katika kizazi hiki.

2 Katika wanyama wote walio safi ujitwalie saba saba, mume na mke; na katika wanyama wasio safi wawili wawili, mume na mke.

3 Tena katika ndege wa angani saba saba, mume na mke; ili kuhifadhi hai mbegu juu ya uso wa nchi yote.

4 Kwa maana baada ya siku saba nitainyeshea dunia mvua, siku arobaini mchana na usiku; na kila kilicho hai nilichokifanya juu ya uso wa nchi nitakifutilia mbali.

5 Nuhu akafanya kama vile Bwana alivyomwamuru.

Tutunze mazingira yetu;

Wanadamu walipoanza kuzidi juu ya uso wa dunia, walitenda uovu. Mungu akaamua kuleta gharika kuwaangamiza. Lakini Nuhu alikuwa mtiifu kwa Bwana, akaelekezwa kutengeneza safina. Sasa katika somo letu Nuhu anaambiwa kuingia kwenye safina aliyokuwa ameitengeneza, yeye na familia yake, na jozi kadhaa za ndege na wanyama. Mungu anasema kuleta mvua kwa siku arobaini itakayoleta gharika.

Mvua ilinyesha dunia ikafunikwa na maji. Wanadamu wote waliangamia, maana miti yote ilianguka. Hata milima yote ilifunikwa na maji. Baada ya mvua kumalizika na maji kupungua, Nuhu na jamaa yake yote walitoka kwenye safina na wanyama na ndege pia waliokuwa kwenye safina. Nuhu alimtolea Mungu sadaka, Mungu akaahidi kutoleta gharika tena.

Mungu anaahidi kutoleta gharika;

Mwanzo 8:21-22

21 Bwana akasikia harufu ya kumridhisha; Bwana akasema moyoni, Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake; wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya.
22 Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma. 

Mungu aliwaangamiza watu ambao hawakumcha akamuokoa Nuhu na jamaa yake kwa sababu ya uchaji wake. Lakini baada ya gharika kama tulivyoona Mungu anaahidi neema kwa wanadamu. Tunayo neema kwa njia ya Yesu Kristo tukimpokea na kumwamini, yeye aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa ajili yetu. Mwamini sasa uokolewe. Amina.

Jumamosi njema.

Heri Buberwa