Ijumaa asubuhi tarehe 12.04.2024
Mwanzo 1:24-31
24 Mungu akasema, Nchi na izae kiumbe hai kwa jinsi zake, mnyama wa kufugwa, nacho kitambaacho, na wanyama wa mwitu kwa jinsi zake; ikawa hivyo.
25 Mungu akafanya mnyama wa mwitu kwa jinsi zake, na mnyama wa kufugwa kwa jinsi zake, na kila kitu kitambaacho juu ya nchi kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.
26 Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.
27 Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.
28 Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.
29 Mungu akasema, Tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu, ulio juu ya uso wa nchi yote pia, na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu;
30 na chakula cha kila mnyama wa nchi, na cha kila ndege wa angani, na cha kila kitu kitambaacho juu ya nchi, chenye uhai; majani yote ya miche, ndiyo chakula chenu; ikawa hivyo.
31 Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita.
Tutunze mazingira yetu;
Kitabu cha Mwanzo huanza kwa kusimulia kuhusu uumbaji wa Mungu. Mstari wa kwanza kabisa huanza kwa kusema "Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi". Asubuhi hii tunasoma mwendelezo wa uumbaji kwa siku ya sita. Mungu anaumba wanyama wa mwituni, wa kufugwa, na watambaao. Katika mstari wa 26 Mungu anaumba mwanadamu kwa mfano wake, mwanamume na mwanamke. Anatoa baraka kwao, kwamba wakazae na kuongezeka wakitawala vitu vilivyoko duniani.
Vitu vingine vyote Mungu aliviumba, lakini alimuumba mwanadamu kwa "mfano wake". Hapa kuna upekee kwa mwanadamu. Siyo hilo tu la kuumbwa kwa mfano wa Mungu, lakini kupewa mamlaka juu ya kila kiendacho juu ya nchi. Huu ni utume kwetu, kwamba tuishi kwa kumpendeza Mungu tukipendana maana tumeumbwa kwa mfano wake. Lakini pia tuitunze dunia tuliyowekwa na Mungu, sisi kama wenye mamlaka juu ya kila chenye uhai juu ya nchi ili dunia iwe salama kwa viumbe vyote. Tukitunza mazingira tunatunza uumbaji wa Mungu. Amina
Ijumaa njema.
Heri Buberwa