Date: 
25-03-2024
Reading: 
Yohana 2:23-25

Juma Takatifu 

Jumatatu asubuhi tarehe 25.03.2024

Yohana 2:23-25

23 Hata alipokuwapo Yerusalemu kwenye sikukuu wakati wa Pasaka, watu wengi waliamini jina lake, walipoziona ishara zake alizozifanya.

24 Lakini Yesu hakujiaminisha kwao; kwa kuwa yeye aliwajua wote;

25 na kwa sababu hakuwa na haja ya mtu kushuhudia habari za mwanadamu; kwa maana yeye mwenyewe alijua yaliyomo ndani ya mwanadamu.

Shangilieni Bwana anakuja;

Yesu alialikwa kwenye harusi moja huko Kana ya Galilaya, wakanywa wakafurahi divai ikaisha. Wakati wanahangaika wapate wapi divai, Yesu akageuza maji kuwa divai. Huu ni mwanzo wa ishara ambayo Yesu aliifanya huko Kana ya Galilaya akaudhihirisha Utukufu wake. 

Baada ya hapo Pasaka ilikuwa inakaribia, Yesu akapanda kwenda Yerusalemu. Akakuta watu wanafanya biashara hekaluni! Akapindua meza zao, akawafukuza akisema nyumba ya Baba yangu ni nyumba ya sala. Iliwakera sana Wayahudi hadi wakamuuliza alifanya vile kwa mamlaka gani? Akawaambia livunjeni hekalu nami nitalijenga ndani ya siku tatu! Walizidi kuchoka, maana hekalu lilijengwa kwa miaka arobaini na sita! Kumbe alinena habari za hekalu la mwili wake.

Ndipo linakuja somo la asubuhi hii, kwamba baada ya hayo yote niliyoeleza hapo juu, watu wakaliamini jina lake. Japokuwa yeye hakujiaminisha kwao, maana aliwajua wote. 

Kumbe ishara alizofanya Yesu zilisababisha wamwamini. 

Nikushawishi na sisi tuendelee kumwamini Yesu kama Mwokozi wetu. Tusiiache imani hii. Sisi tusimfuate kwa ishara, bali kwa imani tukiamini ni Mwokozi wetu. Imani ya kweli itatupa matokeo mazuri daima, hata uzima wa milele. Amina

Uwe na wiki njema

Heri Buberwa Nteboya 

Jumatatu;

Juma Takatifu 2024