Date: 
26-02-2024
Reading: 
Mathayo 14:1-12

Hii ni Kwaresma 

Jumatatu asubuhi 26.02.2024

Mathayo 14:1-12

1 Wakati ule mfalme Herode alisikia habari za Yesu, akawaambia watumishi wake,

2 Huyo ndiye Yohana Mbatizaji; amefufuka katika wafu; na kwa hiyo nguvu hizo zinatenda kazi ndani yake.

3 Maana Herode alikuwa amemkamata Yohana, akamfunga, akamtia gerezani, kwa ajili ya Herodia, mke wa Filipo nduguye.

4 Kwa sababu Yohana alimwambia, Si halali kwako kuwa naye.

5 Naye alipotaka kumwua, aliwaogopa watu, maana walimwona Yohana kuwa nabii.

6 Hata ilipofika sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti Herodia alicheza mbele ya watu, akampendeza Herode.

7 Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lo lote atakaloliomba.

8 Naye, huku akichochewa na mamaye, akasema, Nipe hapa katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji.

9 Naye mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya wale walioketi chakulani pamoja naye, akaamuru apewe;

10 akatuma mtu, akamkata kichwa Yohana mle gerezani.

11 Kichwa chake kikaletwa katika kombe, akapewa yule kijana; akakichukua kwa mamaye.

12 Wanafunzi wake wakaenda, wakamchukua yule maiti, wakamzika; kisha wakaenda wakampasha Yesu habari.

Mawazo maovu ni chanzo cha ukatili;

Yohana alimwambia Herode kuwa ndoa yake na Herodia ilikuwa batili, Herode akamfunga Yohana gerezani. Ilipofika siku ya kuzaliwa kwake, Herode alifanya karamu kubwa. Binti Herodia alicheza vizuri sana akampendeza Herode ambaye alimuahidi kumpa chochote ambacho angeomba. Kwa kushawishiwa na mama yake, Binti Herodia akaomba kichwa cha Yohana. Ilimbidi Herode aamuru Yohana kukatwa kichwa maana alikwisha kuahidi kufanya vile. Lilikuwa ni tendo la kikatili sana. Sasa tuangalie uhusika wa kila mmoja na ujumbe tunaoupata asubuhi hii;

1. Yohana;

Yohana alimwambia Herode kuwa ndoa yake na Herodia mke wa Filipo nduguye ilikuwa batili. Hakuogopa nafasi ya Herode, alimwambia ukweli. Inawezekana Yohana alijua madhara ya kusema hivyo, lakini aliamua kusimama kwa sababu alikuwa akisimamia ukweli.

Yohana anawakilisha kundi la watu wanaoisimamia kweli. Nani leo ni mfano wa Yohana? Anayesimamia ukweli bila kuogopa matokeo yake?

Leo tuna jamii inayokumbatia uovu na kuchekea uongo kwa sehemu kubwa, wengi wakiumia! Tuko tayari kujipendekeza kwa wakubwa tukiutetea uovu huku wengi wakiumia! Huu ni uovu! Huu ni ukatili! Tunajiangalia nafasi zetu tu! Tunasahau wajibu wetu katika kujenga jamii yenye haki!

Lakini pia, tunakemea uovu?

Nani anaisimamia kweli?

Nani anakemea uovu?

Tunaisimamia kweli kama Yohana Mbatizaji?

2. Herode.

Herode alichukia ukweli alioambiwa na Yohana. Alitaka kumuua, lakini kama tulivyoona mwanzo, aliwaogopa watu, na alimwogopa Yohana pia. 

Kuna wachache wakishapewa nafasi hawataki kuambiwa lolote. Wewe nani? Yaani hata uovu usiambiwe? Yaani Herode hakuwa tayari kuambiwa kuhusu ndoa yake batili. Maana yake alitaka kusikia aliyoyataka tu!

Huwezi kuongoza watu usiwasikilize! Huo ni ukatili!

Lakini pia, alitaka kumwua Yohana, na alimuua kwa kutekeleza ahadi yake. Kwa nini kuua? Kwa nini kuua mtu aliyeumbwa kwa mfano wa Mungu? Tumesahau amri ya Mungu ya "usiue"?

Hii roho ya uumbaji haifai!

Lakini pia, Herode anaonekana kuhuzunika sana pale anapoamuru Yohana kukatwa kichwa, akitekeleza ahadi ya binti Herodia. Binafsi naona alikuwa na dhamiri ya kuua, kwa sababu ya yeye kwa nafasi yake, alikuwa na uwezo wa kukataa kutekeleza ahadi ambayo ilikuwa inaondoa uhai wa mtu.

Kwanza, Herode anawakilisha watawala ambao wanatumia nafasi zao kuwaumiza wengine.

Pili, Herode anawakilisha watawala waaoshindwa kutumia mamlaka yao kutenda haki.

Hapa tunaitwa kutokuwa na Roho kama ya Herode, Roho ya kuchukia kuambiwa ukweli, kutokuwa tayari kukosolewa, na kuwa tayari kutekeleza jambo kumfurahisha mtu, wakati mwingine anaumia.

3. Herodia.

Huyu ni muuaji.

Alitaka kumwua Yohana pia. Injili ya Marko inaonesha hili.

Marko 6:19

[19]Naye yule Herodia akawa akimvizia, akataka kumwua, asipate.

Yaani kwa kuambiwa ameolewa na shemeji yake tu, anataka kuua! Halafu binti yake akija kushauriwa zawadi gani aombe, anamwambia aombe kichwa cha Yohana Mbatizaji! Kichwa ni zawadi? 

Yaani anafurahia Yohana akifa!!!?

Yaani kuna baadhi yetu tuko tayari kuwaumiza wenzetu, sababu tu ya furaha zetu za uovu?! 

Huyu ndiye aliyesababisha kifo cha Yohana, kwa maana ya kupendekeza. Asingemwambia binti achague, binti asingemwambia Herode, na Herode asingeamuru Yohana akatwe kichwa. Chanzo ni hapa.

Tafakari;

Wewe umekuwa chanzo cha kuumiza wengine?

4. Binti Herodia.

Huyu alishawishiwa na mama yake aombe kichwa cha Yohana. Na yeye alishiriki kuua, maana asingekubali, Yohana asingekatwa kichwa. Alishiriki kuua.

Sio kila unalolisikia ni sahihi kutenda. Unahitaji kutafakari kwa msaada wa Roho Mtakatifu kabla ya kufikia uamuzi. Unapoambiwa kufanya jambo, fikiria kabla, ili matokeo yake yasiwe yenye kusababisha uovu.

5. Wanafunzi wa Yohana waliuchukua mwili wa Yohana wakauzika, kisha wakaenda kumpasha Yesu habari.

Mathayo 14:12

[12]Wanafunzi wake wakaenda, wakamchukua yule maiti, wakamzika; kisha wakaenda wakampasha Yesu habari.

Kwa kufiwa na Mwalimu wao, walisumbuka nafsi, na kuona njia pekee ya kupata faraja ni kumwendea Yesu na kumpa habari.

Wanatukumbusha kumwendea Yesu nyakati zote, ili atusaidie na kutuwezesha kuondoa uovu na ukatili wa aina zote katika jamii.

Asubuhi hii tunaona familia iliyosababisha kifo cha Yohana Mbatizaji. Inatukumbusha wajibu wetu katika kutenda haki, na kutowaumiza wasio na hatia, maana Yesu alileta haki na amani kwa wote.

Nini nafasi yako katika kupambana na ukatili?

Tunakutakia wiki njema

Heri Buberwa