Event Date: 
21-01-2024

Siku ya Jumapili tarehe 21 Januari 2024, Washarika wa Kanisa Kuu Azania Front waliungana na na jumuiya ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) katika ibada maalum ya kumwingiza kazini Mkuu Mpya wa Kanisa, Baba Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa iliyofanyika katika viwanja vya Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alikuwa mgeni rasmi katika ibada hiyo maalum ambayo pia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa, serikali, wanadiplomasia, viongozi wa taasisi nyingine za kidini pamoja na viongozi na maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri kutoka ndani na nje ya nchi.

Akiongoza ibada hiyo maalum, Mkuu wa KKKT aliyemaliza muda wake, Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo ambaye pia ni Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini alisema ameliacha kanisa katika mikono salama (ya Dkt. Malasusa) na kwamba sasa anaenda kutumia muda wake mwingi katika kuwatumikia washarika wa Dayosisi ya Kaskazini kwa ukaribu zaidi.

Katika salaam zake kwa washarika, Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo aliwashukuru watu na taasisi mbalimbali zilizompa ushirikiano wakati wa uongozi wake kama mkuu wa kanisa. Pia aliomba ushirikiano huo uendelezwe kwa mkuu mpya wa kanisa.

Baba Askofu Dkt Malasusa, nakupongeza kwa kupewa (nafasi ya kuwa Mkuu wa Kanisa) kwa mara nyingine kuliongoza Kanisa la Kiinjili la Kulutheri Tanzania, ninakuombea sana kwa Mungu akujalie afya njema, hekima, busara na unyenyekevu ili uliongoze Kanisa la Mungu kwa utukufu wake. Msikilize huyu aliyekuita na kukupa nafasi hii, usiingie katika jaribu la kusema mbwa mzee hafundiswi tena namna mpya ya kuwinda. Wewe msikilize roho mtakatifu, msikilize aliyekuita, yeye anasema ‘nitakushauri na kukuonyesha njia utakayoiendea’. Nina uhakika ukimsikiliza Mungu unayemtegema basi utumishi wako utakuwa heri na wa baraka; na Kanisa zima la Kiinjili la Kilutheri Tanzania litazidi kustawi,” alisema Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo.

Kwa upande wake Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Jerusalem India, Dkt. Christian Samraj alimtaka Mkuu Mpya wa KKKT (Dkt. Malasusa) kuhakikisha anatenda haki na kushughulikia changamoto zinazoikumba dunia kwa sasa.

Hata sasa ulimwengu una changamoto na katika hizo Dkt. Malasusa umeitwa kukabiliana nazo na kutumia mamlaka ambayo Mungu mwenyewe amekupa. Umetakiwa uzae matunda katika uongozi wako na yadumu milele,” alisema Dkt. Samraj.

Katika hotuba yake, Mkuu Mpya wa Kanisa, Baba Askofu Dkt. Alex Malasusa alimpongeza Baba Askofu aliyemaliza Muda wake Dkt. Fredrick Shoo kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya kwa kanisa wakati wa uongozi wake na kuahidi kwamba ataendeleza mema yote ambayo mtangulizi wake aliyaanzisha.

Namshukuru sana Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo kwa mengi sana aliyoyafanya na kuyakamilisha wakati wa kipindi chake. Mimi nitaendeleza pale alipoishia maana kanisa la Mungu halina awamu. Kanisa na wito wake ni endelevu hadi pale Bwana Yesu atakaporudi kulichukua. Kwa kusema hivi nawaomba maaskofu wenzangu na viongozi wengine wa kanisa, watumishi na washarika wote tushirikiane kulinda na kuimarisha umoja wa kanisa la Mungu,” alisema Baba Askofu Malasusa.

Akizungumza katika ibada hiyo maalum, Mgeni rasmi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alimpongeza Dkt. Malasusa kwa kuchaguliwa kuwa Mkuu wa Kanisa na kumtakia kila la kheri katika utumishi wake. Akitumia maneno kutoka kitabu kitakatifu cha Biblia, Kumbukumbu la Torati 31: 8; Naye BWANA, yeye ndiye atakayekutangulia, atakuwa pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha; usiogope wala usifadhaike. Rais Samia alimpongeza na kumtia moyo mkuu mpya wa kanisa na kumwomba awe baraka kwa kanisa, waumini na taifa kwa ujumla.

Natambua Baba Askofu (Dkt. Malasusa) kuwa pamoja na kuwa muumini mzuri na msomi hodari wa theolojia uliwahi pia kuwa Mkuu wa KKKT kati ya mwaka 2007 hadi 2015 pale ulipopokea kijiti kutoka kwa Askofu Samson Mshemba, Mwenyezi Mungu amrehemu. Natambua pia kuwa ulikuwa mkuu wa KKKT wa kwanza mwenye umri mdogo kuliko wote kuwahi kuliongoza kanisa ukiwa na umri wa miaka 47 tu, hivyo kuchaguliwa kwako kwa mara nyingine hakujaja kwa bahati mbaya bali kumetokana na historia yako na ukomavu wako katika uongozi wa kanisa. Vilevile kunadhihirisha imani na tathimini au thamani ya viongozi na waumini wenzio waliyonayo juu yako. Hongera sana Baba Askofu Malasusa, ni dhahiri kwamba una uzoefu, uwezo na uelewa mkubwa kuhusu misingi na mifumo ya uendeshaji wa kanisa hili. Hivyo waumini wa kanisa hili na wananchi kwa ujumla watanufaika sana na ubobezi wako,’’ alisema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia alisema serikali itaendelea kuimarisha huduma za ustawi wa jamii na kushirikiana na wadau wengine zikwemo taasisi za kidini ili kuhakikisha huduma hizo zinapatikana. Rais Samia aliongeza kusema kuwa taasisi za dini zina mchango mkubwa katika kuwajenga waumini kiimani na kujenga taifa lenye watu wema, wanaowajibika katika jamii na kuwa wastahimilivu zinapotokea changamoto.

Mkuu wa Kanisa Mpya, Baba Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa ambaye pia ni Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, alichaguliwa kwa kishindo na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 21 wa KKKT uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Makumira jijini Arusha tarehe 25 Agosti 2023. Hii ni mara ya pili kwa Dkt. Malasusa kuchaguliwa kuwa Mkuu wa Kanisa, kwani amewahi kuhudumu katika nafasi hiyo kati ya mwaka 2007 mpaka mwaka 2015.

Baadhi ya matukio katika Picha wakati wa Ibada Maalum ya kuingizwa kazini rasmi kwa Mkuu mpya wa Kanisa. Picha: Ikulu Tanzania

Rais Samia Suluhu Hassan akipokea zawadi ya picha kutoka kwa Mkuu Mpya wa KKKT Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa mara baada ya Ibada Maalum ya Kumuingiza kazini Askofu huyo iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Azania Front Jijini Dar es Salaam tarehe 21 Januari, 2024.

Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia wageni, viongozi mbalimbali pamoja na Washarika wa Kanisa la Azania Front wakati wa Ibada Maalum ya Kumuingiza kazini Mkuu Mpya wa KKKT Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa iliyofanyika Kanisani hapo Jijini Dar es Salaam 21 Januari, 2024.

Mkuu Mpya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa akizungumza wakati wa Ibada Maalum ya Kumuingiza kazini iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Azania Front Jijini Dar es Salaam tarehe 21 Januari, 2024.

Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye Ibada Maalum ya Kumuingiza kazini Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa inayofanyika Kanisani hapo Jijini Dar es Salaam tarehe 21 Januari, 2024

Baadhi ya Wachungaji wakiwa kwenye Ibada Maalum ya Kumuingiza kazini Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa inayofanyika Kanisani hapo Jijini Dar es Salaam tarehe 21 Januari, 2024.

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza jambo na Watoto waliohudhuria Ibada Maalum ya Kumuingiza kazini Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa inayofanyika Kanisani hapo Jijini Dar es Salaam tarehe 21 Januari, 2024.

 

Tazama ibada hiyo maalum kupitia Azania Front TV: https://www.youtube.com/watch?v=IdP3QuomxcA