Jumatano asubuhi tarehe 27.12.2023
1 Timotheo 1:12-17
12 Nami namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu kwa sababu aliniona kuwa mwaminifu, akaniweka katika utumishi wake;
13 ingawa hapo kwanza nalikuwa mtukanaji, mwenye kuudhi watu, mwenye jeuri, lakini nalipata rehema kwa kuwa nalitenda hivyo kwa ujinga, na kwa kutokuwa na imani.
14 Na neema ya Bwana wetu ilizidi sana, pamoja na imani na pendo lililo katika Kristo Yesu.
15 Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi; ambao wa kwanza wao ni mimi.
16 Lakini kwa ajili hii nalipata rehema, ili katika mimi wa kwanza, Yesu Kristo audhihirishe uvumilivu wake wote; niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini baadaye, wapate uzima wa milele.
17 Sasa kwa Mfalme wa milele, asiyeweza kuona uharibifu, asiyeonekana, Mungu peke yake, na iwe heshima na utukufu milele na milele. Amina.
Tunaitwa kuwa Mashahidi wa Kristo;
Asubuhi hii tunamsoma Mtume Paulo akimshukuru Kristo kwa kumfanya mtumishi wake, japokuwa alikuwa akitenda uovu hapo mwanzo. Ndipo Paulo anasema Kristo alikuja ulimwenguni kuwaokoa wenye dhambi. Anampa utukufu na heshima, yeye aliye Mwokozi wa wote.
Paulo anamtuma Timotheo kupeleka ujumbe huu kwa watu, kwamba Yesu Kristo ndiye Mwokozi wa ulimwengu. Ujumbe huu unakuja kwetu asubuhi hii ukituita kumpokea Yesu mioyoni mwetu, na kuwa mashaidi wake daima. Tunakuwa mashahidi wa Kristo kwa kufanya yale anayotutuma, yaani kuwa na imani, toba na msamaha katika yeye. Ushuhuda wetu utawaleta wengine kwake, na huu ndiyo utume wetu katika yeye. Wewe ni shahidi wa Kristo?
Jumatano njema
Heri Buberwa