Date: 
23-11-2023
Reading: 
Isaya 29:18-24

Alhamisi asubuhi tarehe 23.11.2023

Isaya 29:18-24

18 Na katika siku hiyo viziwi watasikia maneno ya hicho chuo, na macho ya vipofu yataona katika upofu na katika giza.

19 Wanyenyekevu nao wataongeza furaha yao katika Bwana, na maskini katika wanadamu watafurahi katika Mtakatifu wa Israeli.

20 Kwa maana mwenye kutisha ameangamizwa, naye mwenye dharau amekoma, nao wote watazamiao uovu wamekatiliwa mbali;

21 hao wamfanyao mtu kuwa amekosa katika neno, na kumtegea mtego yeye aonyaye langoni, na kumgeuza mwenye haki kwa kitu kisichofaa.

22 Basi, Bwana aliyemkomboa Ibrahimu asema hivi, katika habari za nyumba ya Yakobo; Yakobo hatatahayarika sasa, wala uso wake hautabadilika rangi yake.

23 Bali atakapowaona watoto wake, walio kazi ya mikono yangu, katikati yake, wao watalitakasa jina langu; naam, watamtakasa Mtakatifu wa Yakobo, nao watamcha Mungu wa Israeli.

24 Hao nao wakosao rohoni mwao watapata kufahamu, na hao wanung'unikao watajifunza elimu.

Hukumu ya mwisho inakuja;

Ni ujumbe wa Bwana kupitia kwa Nabii Isaya kuhusu siku zijazo kwa wana wa Israeli. Kumbuka ujumbe huu walipewa wakiwa kabla hawapelekwa uhamishoni. Kama tulivyosoma, tunaona wakiambiwa kuwa wakisikia neno la Mungu na kuwa wanyenyekevu wataongeza furaha yao. Mkazo wa Isaya ni watu kupata ufahamu kwa kumwamini Bwana.

Pamoja na Israel kupitia nyakati tofauti, Bwana hakuacha kuwa nao. Lakini muhimu zaidi ni kuwa Bwana hakuacha kuwaelekeza waishi vipi ili wadumu katika yeye. Mungu hufanya hivi hata sasa, akituita kumwamini kwa njia Yesu Kristo aliye Mwokozi wa ukimwengu. Tukimwamini huyu Kristo tutaurithi uzima wa milele. Amina.

Alhamisi njema.

 

Heri Buberwa