Jumanne asubuhi tarehe 07.11.2023
Danieli 12:5-13
5 Ndipo mimi, Danielii, nikatazama, na kumbe, wamesimama wengine wawili, mmoja ukingoni mwa mto upande huu, na mmoja ukingoni mwa mto upande wa pili.
6 Na mmoja akamwuliza yule mtu aliyevikwa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto, Je! Itakuwa muda wa miaka mingapi hata mwisho wa mambo haya ya ajabu?
7 Nami nikamsikia yule mtu aliyevikwa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto, hapo alipoinua mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto kuelekea mbinguni; akaapa kwa yeye aliye hai milele na milele, ya kwamba itakuwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati; tena watakapokuwa wamekwisha kuvunja nguvu za hao watu watakatifu, ndipo mambo hayo yote yatakapotimizwa.
8 Nami nikasikia, lakini sikuelewa; ndipo nikasema, Ee Bwana wangu, mwisho wa mambo haya utakuwaje?
9 Akasema, Enenda zako, Danielii; maana maneno haya yamefungwa, na kutiwa muhuri, hata wakati wa mwisho.
10 Wengi watajitakasa, na kujifanya weupe, na kusafika; bali wabaya watatenda mabaya; wala hataelewa mtu mbaya awaye yote; bali wao walio na hekima ndio watakaoelewa.
11 Na tangu wakati ule ambapo sadaka ya kuteketezwa ya daima itaondolewa, na hilo chukizo la uharibifu litakaposimamishwa, itapata siku elfu na mia mbili na tisini.
12 Heri angojaye, na kuzifikilia siku hizo elfu na mia tatu na thelathini na tano.
13 Lakini enenda zako hata utakapokuwa mwisho ule; maana wewe utastarehe, nawe utasimama katika kura yako mwisho wa siku hizo.
Uenyeji wa mbinguni;
Nabii Danieli anatoa unabii wa yajayo baada ya maisha ya duniani. Ukianzia nyuma kidogo unaona akisema;
Danieli 12:2
Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele.Katika somo Daniel anaeleza kuwa wapo watakaotenda mema, na wapo watakaotenda mabaya pia. Lakini anasema heri astahimiliye katika Bwana maana mwisho wake utakuwa katika Bwana.
Unabii wa Danieli unatiliwa mkazo na Yesu Kristo tuliyempokea, ambaye hutualika kwake daima ili atupe uzima wa milele. Kristo anatuita kudumu katika neema yake, ili kwa imani tutende mema na hatimaye tuurithi uzima wa milele. Amina.
Siku njema
Heri Buberwa