Date:
05-10-2023
Reading:
Mithali 22:15
Alhamisi asubuhi 05.10.2023
Mithali 22:15
Ujinga umefungwa ndani ya moyo wa mtoto; Lakini fimbo ya adhabu itaufukuzia mbali.
Tuwalee watoto katika njia ya Bwana;
Asubuhi hii tunasoma juu ya ujinga kufungwa ndani ya mtoto. Maana yake ni kuwa watoto kwa sababu ya udogo wao, hawajui mambo yanayohusu maisha kwa ujumla. Hivyo wanahitaji kujifunza, na kwa sababu ya udogo wao wanatakiwa kufundishwa. Mwandishi anatumia lugha ya "fimbo ya adhabu" kufukuza ujinga kwa mtoto kwa maana ya kuhakikisha mtoto anafundishwa mambo yampasayo kujua na kutenda katika Kristo.
Wajibu wetu kama familia, jamii na Kanisa kwa ujumla ni kuhakikisha tunaondoa ujinga kwa watoto wetu. Tuondoe ujinga wa kutomjua Mungu kwa kuwawekea mazingira ya kulijua neno la Mungu kama msingi wa maisha yao. Huo ndiyo urithi bora kwa watoto wetu kama Kanisa la sasa na baadaye. Amina.
Alhamisi njema.
Heri Buberwa