22 Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana,
23 (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana),
24 wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili.
Uwakili wetu kwa Bwana;
Baada ya Yesu kuzaliwa na kutimiza siku nane alipelekwa hekaluni kama ilivyokuwa desturi toka enzi za Agano la kale. Luka anarejea Agano la kale kuonesha Yesu alivyopelekwa hekaluni.
Angalia rejea ya Luka;
Mambo ya Walawi 12:6-8
6 Kisha hizo siku za kutakaswa kwake zitakapotimia, kwa ajili ya mwana, au kwa ajili ya binti, ataleta mwana-kondoo wa mwaka mmoja kuwa sadaka ya kuteketezwa na kinda la njiwa, au hua, kuwa sadaka ya dhambi, awalete mlangoni pa hema ya kukutania, na kumpa kuhani;
7 na yeye atawasongeza mbele za Bwana, na kufanya upatanisho kwa ajili yake; naye atatakasika na jicho la damu yake. Hii ndiyo amri yake huyo azaaye, kwamba ni mtoto mume au mke.
8 Kama mali yake huyo mwanamke haimfikilii mwana-kondoo, hapo ndipo atakapochukua hua wawili, au makinda mawili ya njiwa; mmoja kuwa sadaka ya kuteketezwa, na wa pili kuwa sadaka ya dhambi; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atakuwa safi.
Soma tena hapa;
Kutoka 13:2, 13
2 Nitakasie mimi wazaliwa wa kwanza wote, kila afunguaye tumbo katika wana wa Israeli, wa binadamu na wa mnyama; ni wangu huyo.
13 Kila mzaliwa wa kwanza wa punda utamkomboa kwa mwana-kondoo; na kwamba hutaki kumkomboa, utamvunja shingo; na kila mzaliwa wa kwanza wa binadamu katika wanao utamkomboa.
Kumbe ilikuwa Agizo kwa watoto waliozaliwa kupelekwa hekaluni. Kwa kutambua kuwa lilikuwa Agizo la Bwana, wazazi hawakuacha kuwapeleka watoto wao hekaluni kwa utakaso kama ambavyo tumesoma Yesu akipelekwa.
Wazazi wa Yesu walitimiza agizo la Mungu kwa kumpeleka Yesu hekaluni. Agizo la Mungu kwa mwanadamu kuishi akimcha halijawahi kubadilika, liko pale pale. Tunakumbushwa kuishi tukimcha Bwana katika maisha yetu, tukikumbuka kuwa vitu vyote tulivyo navyo ni mali yake. Hivyo tuwe mawakili wema katika vitu vyote alivyotupa. Amina.
Siku njema.
----------------------------------
Heri Buberwa
Mlutheri