Date: 
04-09-2023
Reading: 
Kumbukumbu la Torati 27:17-19

Jumatatu asubuhi tarehe 04.09.2023

Kumbukumbu la Torati 27:17-19

17 Na alaaniwe aondoaye mpaka wa jirani yake. Na watu wote waseme, Amina.

18 Na alaaniwe ampotezaye kipofu akakosa njia. Na watu wote waseme, Amina.

19 Na alaaniwe apotoaye hukumu ya mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe. Na watu wote waseme, Amina.

Jirani wetu;

Tunaanza juma kwa ujumbe wa Musa akiwaagiza Walawi kuwaambia Israeli yawapasayo kutenda katika kuishi kwao. Anawaelekeza mambo wasiyotakiwa kufanya. Sehemu tuliyosoma inatoa laana kwa aondoaye mpaka wa jirani yake, ampotezaye kipofu, nao apotoaye hukumu ya mgeni, yatima na mjane. Kwa sehemu hii Musa anatuma ujumbe wa kuacha kuonea jirani, bali kuwapenda. 

Kinyume cha laana ni baraka. Ndiyo maana baada ya laana katika sura ya 27, Musa anatangaza baraka za Mungu kwa wote watakaomcha Bwana katika sura ya 28.

Ujio wa Kristo ulilenga kuitimiliza torati. Ndiyo maana Yesu aliitimiliza torati kwa kusisitiza upendo kwa jirani;

Mathayo 22:39

Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako.

Ni agizo la Yesu Kristo kwetu kuwapenda jirani zetu. Jirani yako ni mtu yeyote, hivyo watendee watu wote wema. Hiyo ni amri, kwamba tuwapende jirani zetu. Amina.

Uwe na wiki njema ukiwapenda jirani zako.

Heri Buberwa