Date: 
01-08-2023
Reading: 
Ezekiel 33:1-9

Jumanne asubuhi tarehe 01.08.2023

Ezekieli 33:1-9

1 Neno la Bwana likanijia, kusema,

2 Mwanadamu, sema na wana wa watu wako, uwaambie, Hapo nitakapoleta upanga juu ya nchi, watu wa nchi hiyo wakimtwaa mtu mmoja miongoni mwao, na kumweka awe mlinzi wao;

3 ikiwa, aonapo upanga unakuja juu ya nchi hiyo, apiga tarumbeta na kuwaonya watu;

4 basi mtu awaye yote aisikiaye sauti ya tarumbeta, wala haonywi, upanga ukija na kumwondoa, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe.

5 Aliisikia sauti ya tarumbeta, wala hakuonywa; damu yake itakuwa juu yake; lakini kama angalionywa, angalijiokoa roho yake.

6 Bali mlinzi akiona upanga unakuja, kama hapigi tarumbeta, wala watu hawakuonywa, na upanga ukaja ukamwondoa mtu awaye yote miongoni mwao; ameondolewa huyo katika uovu wake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwa mlinzi huyo.

7 Basi wewe, mwanadamu, nimekuweka kuwa mlinzi kwa nyumba ya Israeli; basi ulisikie neno hili kinywani mwangu, ukawape maonyo yangu.

8 Nimwambiapo mtu mbaya, Ewe mtu mbaya, hakika utakufa, nawe husemi neno la kumwonya mtu huyo, aiache njia yake, mtu mbaya huyo atakufa katika uovu wake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako.

9 Walakini ukimwonya mtu mbaya kwa sababu ya njia yake, kusudi aiache; wala yeye asiiache; atakufa huyo katika uovu wake, lakini wewe umejiokoa roho yako.

Wema wa Mungu watuvuta tupate kutubu;

Asubuhi ya leo tunamsoma Nabii Ezekieli akionya juu ya upanga toka kwa Bwana kwa wote waliomkosea Mungu. Anawaita watu kuisikia sauti ya Mungu inayowaita kutoka upotevuni. Katika mstari wa tisa Nabii Ezekieli anasisitiza kuwa asiyeisikia sauti ya Mungu atakufa katika uovu.

Ujumbe wa asubuhi ya leo ni kuisikia sauti ya Mungu na kutubu dhambi. Sauti ya Mungu inatujia kwa njia ya neno lake. Tunapolisoma na kulisikia neno la Mungu tunawajibika kulishika. Tunapolishika neno lake anakaa kwetu. Matokeo ya kutoisikia sauti ya Mungu ni kuangamia. Amina.

Jumanne njema.

 

Heri Buberwa