Event Date: 
16-07-2023

Siku ya Jumapili tarehe 16 Julai 2023 ilikuwa ni siku ya Vijana katika Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front Cathedral, siku ambayo huadhimishwa kila mwaka ili kutambua na kuthamini mchango wa vijana katika kulijenga na kuliendeleza neno la Bwana.

Katika siku hiyo muhimu kwa vijana na usharika kwa ujumla, vijana wa Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front Cathedral walipata fursa ya kuongoza ibada zote tatu za siku hiyo zilizoambatana na uimbaji na igizo fupi. Akitoa mahubiri ya siku hiyo kwa ibada za Kiswahili, Bi Upendo Makundi, ambaye pia ni Katibu wa Umoja wa Vijana wa Usharika aliwaasa washarika hususani vijana kusimama katika Imani na kuwa hodari katika kuyatenda yale yampendezayo Mungu.

“Tumwamwini Yesu Kristo, sisi huwa tunazaliwa katika utumwa wa dhambi, yatupasa sasa kuwa hodari kushinda hiyo dhambi. Simama, tetea imani yako na uwe hodari. Sisi ni wenye dhambi hivyo yatupasa kila siku iitwayo leo kukiri na kutubu dhambi zetu na kurejea kwa Mungu,” alisema.

Bi Upendo Makundi wakati akihubiri katika moja ya ibada za Kiswahili zilizofanyika Usharikani Azania Front Cathedral, 16 Julai 2023.

“Ungekuwa na maarifa ya neno la Mungu leo hii usingekuwa unatangatanga. Vijana wenzangu tuache kutangatanga, tusimame katika Imani zetu na tuwe hodari. Tusipende mambo ya fasta fasta, fanya kazi. Acha habari za kuambiwa kuwa ukienda kwa nabii fulani utapata gari, hakuna gari la kuokota na hakuna pesa ya bure. Fanya kazi na asiyetaka kufanya kazi na asile. Kwahiyo vijana nawaasa, nawaomba tumtegemee Mungu atatushindia,” aliongeza.

Akizungumza katika ibada hiyo Mchungaji Joseph Mlaki aliwapongeza vijana kwa kujitokeza kwa wingi katika ibada zote tatu na kushiriki kikamilifu katika kuendesha ibada hizo.

Mbali na kuendesha ibada za siku nzima ya Jumapili, siku ya vijana iliendelea alasiri ambapo tamasha la uimbaji lilifanyika likizihusisha kwaya na vikundi vya burudani vya Umoja wa Vijana wa Usharika huku kwaya za vijana za sharika jirani pia zikialikwa kutumbuiza.

Neno na mafundisho katika siku ya vijana mwaka 2023 yalitoka katika kitabu cha Kumb. 31: 6 -8 yakibebwa na kichwa cha neno kisemacho Kijana Uwe Hodari Katika Imani”

Picha zaidi kutoka kwenye Ibada za Siku ya Vijana Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front Cathedral.

Ibada zote tatu pamoja na igizo fupi la siku hiyo zilirushwa moja kwa moja kupitia YouTube chaneli ya Azaniafront TV; kama ulikosa mataukio yote ya siku hiyo unaweza kuyatazama kupitia link zifuatazo;

TAZAMA MATUKIO YOTE HAPA.

Ibada ya Kwanza - Kiswahili

Ibada ya Pili - English Service

Ibada ya Tatu - Kiswahili