Date: 
27-05-2023
Reading: 
Mathayo 8:1-4

Jumamosi asubuhi tarehe 27.05.2023

Mathayo 8:1-4

1 Naye aliposhuka mlimani, makutano mengi walimfuata.

2 Na tazama, akaja mtu mwenye ukoma akamsujudia, akisema, Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa.

3 Yesu akanyosha mkono, akamgusa, akisema Nataka; takasika. Na mara ukoma wake ukatakasika.

4 Yesu akamwambia, Angalia, usimwambie mtu; ila enenda zako, ukajionyeshe kwa kuhani, ukaitoe sadaka kama alivyoamuru Musa, iwe ushuhuda kwao.

Usikie kuomba kwetu;

Baada ya hotuba ya mlimani Yesu alishuka mlimani. Ndipo mwenye ukoma alimjia akiomba kutakaswa, na Yesu akamtakasa kwa neno lake. Mistari hii inatuonesha mambo mawili;

Yule mwenye ukoma alitambua kuwa angeenda kuomba utakaso kwa Yesu angeponywa. Aliamua kwenda akamsujudia Yesu akiomba kutakaswa. Yesu alisikia kuomba kwake. Hapa tunafundishwa kumuomba Yesu, maana yeye husikia kuomba kwetu.

Lakini pia, Injili ni maisha halisi. Yesu alimwambia aliyetakasika arudi kwa makuhani maana ndiyo waliomfahamu, akatoe sadaka huko. Tofauti na siku hizi, mkutano uko Kawe, mhubiri ni wa Dodoma, aliyeponywa ni wa Kibiti, sadaka inatolewa Magomeni. Hakuna anayemjua mwingine! Inatufundisha kumwamini na kumfuata Yesu peke yake, tuepuke mafundisho yasiyofaa. 

Tumwamini Yesu na kumuomba bila kuchoka, maana yeye husikia kuomba kwetu. Jumamosi njema.

 

Heri Buberwa